Joy FM
Joy FM
5 September 2026, 14:28

Hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Kigoma Maweni imepokea mashine kwa ajili ya watoto njiti kutoka taasisi ya kupambana na kuzuia rushwa TAKUKURU
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) imekabidhi mashine mbili maalum kwa ajili ya kusaidia utoaji wa huduma kwa watoto waliozaliwa kabla ya muda, maarufu kama watoto njiti, katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kigoma Maweni.

Mashine hizo zimetolewa kupitia michango binafsi ya watumishi wa TAKUKURU, ikiwa ni sehemu ya juhudi za taasisi hiyo katika kuunga mkono huduma za kijamii na kugusa maisha ya wananchi katika mikoa mbalimbali ya Tanzania Bara.
Akizungumza katika hafla fupi ya kupokea vifaa hivyo, Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Balozi Simon Sirro, amewataka wazazi kuhakikisha wanahudhuria kliniki kwa wakati ili kubaini mapema changamoto zinazoweza kujitokeza wakati wa ujauzito na kujifungua, hatua ambayo inaweza kusaidia kunusuru maisha ya mama na mtoto.

Balozi Sirro pia ameitaka jamii kuachana na imani potofu kuhusu watoto njiti na badala yake kuwapatia watoto hao huduma stahiki za kiafya.
Aidha, amewataka wanaume, hususan wakina baba, kushiriki kikamilifu katika kuhakikisha uzazi salama kwa kuwasaidia wake zao kupata huduma za afya na kutoruhusu kujifungua nyumbani bila usimamizi wa wataalamu wa afya.
“Ni muhimu kuhakikisha mama anapata huduma za afya kwa wakati ili kupunguza hatari zinazoweza kujitokeza wakati wa ujauzito na kujifungua,” amesema Balozi Sirro.

Mkuu huyo wa Mkoa ameishukuru TAKUKURU kwa kugusa maisha ya wananchi wa Kigoma na Tanzania kwa ujumla kupitia hatua hiyo, akisema mchango huo unaunga mkono juhudi za Serikali katika kuboresha huduma za afya nchini.
Kwa upande wake, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Neema Mwakalyelye, amesema mashine hizo zina kazi tofauti, ambapo moja itatumika kusaidia kuongeza joto kwa watoto njiti, huku nyingine ikiwa maalum kwa ajili ya kuwasaidia watoto wenye changamoto ya homa ya manjano.
Mwakalyelye amesema TAKUKURU imeendelea na mpango wa kuchangia vifaa hivyo katika hospitali za mikoa mbalimbali nchini, ambapo tayari mashine hizo zimetolewa katika mikoa 25, huku Kigoma ikiwa mkoa wa 26 kunufaika na mpango huo.
Amesema lengo la taasisi hiyo ni kuhakikisha mpango huo unafikia mikoa yote ya Tanzania Bara ili kuongeza uwezo wa hospitali katika kutoa huduma kwa watoto waliozaliwa kabla ya muda.
“Mashine hizi zimenunuliwa kupitia michango binafsi ya wafanyakazi wa taasisi hii, ikiwa ni sehemu ya mchango wao binafsi katika kuigusa jamii,” amesema Mwakalyelye.
Hatua hiyo inatarajiwa kuongeza uwezo wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kigoma Maweni katika kuwahudumia watoto njiti na kupunguza changamoto zinazoweza kuhatarisha maisha yao.