Joy FM
Joy FM
21 July 2026, 09:25

Kutoa misaada kwa wagonjwa waliolazwa hospitalini ni kitendo cha huruma, upendo na mshikamano kinachochangia kuboresha ustawi wa wagonjwa na familia zao na misaada hiyo inaweza kujumuisha vyakula, sabuni, nguo, vifaa vya usafi na mahitaji mengine muhimu yanayosaidia kurahisisha maisha ya wagonjwa wakati wa matibabu.
Na Hagai Ruyagila
Maafisa usafirishaji (bodaboda) katika stendi kuu ya mabasi Kasulu mjini wametoa msaada wa vitu mbalimbali, kwa wagonjwa waliolazwa katika wodi ya watoto Hospitali ya Mlimani, Halmashauri ya Mji Kasulu mkoani Kigoma.

Akizungumza wakati wa kukabidhi Msaada huo Bakari Miraji Rashidi Mwenyekiti wa maafisa usafirishaji hao amesema wataendelea kutoa msaada kwa wahitaji mbalimbali ili kuwapa faraja na kuwatia moyo.
Mkuu wa usalama barabarani wilaya ya Kasulu, Mrakibu wa polisi Patrick Damas, amewapongeza waendesha bodaboda hao kwa wazo lao la kuwajali wagonjwa, akieleza kuwa kitendo hicho ni mfano mzuri unaopaswa kuigwa na makundi mengine katika jamii.

Mkaguzi Msaidizi wa Polisi na Polisi Kata wa Nyamnyusi, Willy Lupa, amewataka maafisa usafirishaji hao kuendelea kudumisha amani, upendo na mshikamano.

Kaimu Muuguzi mfawidhi hospital ya Mlimani halmashauri ya Mji kasulu Magreth Nyamuhanga ameeleza namna walivyopokea msaada huo kwa ajili ya wagonjwa.

Baadhi ya wazazi wa watoto waliopokea msaada huo wametoa shukrani kwa maafisa usafirishaji hao amaarufu bodaboda kwa moyo wao wa kujitolea, huku wakisema utawasaidia kutatua baadhi ya changamoto mbalimbali.
