Joy FM

Serikali kukamilisha mfumo wa kufuatilia taarifa za mabaharia Nchini

22 June 2026, 16:35

Baadhi ya viongozi mbalimbali wakiwa katika uzinduzi wa maadhimisho ya mabaharia ambayo yamefanyika kitaifa Mkoani Kigoma, Picha Hamis Ntelekwa

Mabaharia ni watu wanaofanya kazi katika vyombo vya usafiri wa majini kama vile meli, boti, na majahazi na wmabaharia wamekuwa wakichangia katika usafirishaji wa watu na bidhaa kutoka sehemu moja kwenda nyingine kupitia bahari, maziwa, na mito na kuchochea maendeleo yanuchumi wao na Taifa kwa ujumla

Na Tryphone Odace

Serikali kupitia Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) kwa kushirikiana na Mamlaka ya Usafiri wa Bahari Zanzibar (ZMA), imesema inaendelea kukamilisha maandalizi ya mfumo wa kidijitali wa kusimamia taarifa za mabaharia nchini, kwa lengo la kuwafuatilia, kutambua changamoto zinazowakabili na kuzitafutia ufumbuzi.

Kauli hiyo imetolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Ally Said, wakati wa uzinduzi wa maadhimisho ya 16 ya Mabaharia uliofanyika kitaifa mkoani Kigoma.

Sauti ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Ally Said, Picha na Hamis Ntelekwa

Amesema mabaharia wamekuwa wakikumbana na changamoto mbalimbali katika utekelezaji wa majukumu yao, hivyo mfumo huo utasaidia serikali kuwa na taarifa sahihi na za wakati kuhusu ustawi wao.

Sauti ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Ally Said

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Mamlaka ya Usafiri wa Bahari Zanzibar (ZMA), Mtumwa Saidi, amesema serikali itaendelea kuboresha mazingira ya kazi kwa mabaharia kwa kuhakikisha sheria, kanuni na miongozo ya sekta hiyo inasimamiwa ipasavyo ili waweze kufanya kazi katika mazingira salama na rafiki.

Sauti ya Mkurugenzi wa Mamlaka ya Usafiri wa Bahari Zanzibar (ZMA), Mtumwa Saidi
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) Nahodha. Mussa Mandia, Picha na Hamis Ntelekwa

Awali akizungumza katika uzinduzi huo, Katibu Tawala wa Mkoa wa Kigoma, Hassan Rugwa, amesema serikali imeendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo katika sekta ya usafirishaji, hatua ambayo imechangia kuimarisha usalama na ufanisi wa huduma za usafiri majini nchini.

Sauti ya Katibu Tawala wa Mkoa wa Kigoma, Hassan Rugwa

Siku ya Mabaharia Duniani huadhimishwa Juni 25 ya kila mwaka na nchi wanachama wa Shirika la Kimataifa la Bahari, IMO, kwa lengo la kutambua mchango wa mabaharia katika sekta ya usafirishaji wa majini. Mwaka huu, maadhimisho hayo yamebeba kaulimbiu isemayo; “Kutoka Sera hadi Utekelezaji: Kuimarisha Ubora katika Sekta ya Usafiri Majini.”