Joy FM
Joy FM
23 July 2026, 13:41

Hati safi ni maoni yanayotolewa na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali baada ya kufanya ukaguzi wa taarifa za fedha za halmashauri na kubaini kuwa zimeandaliwa kwa usahihi na kwa kuzingatia sheria, kanuni, na viwango vya uhasibu vinavyotumika na kupata hati safi ni ishara ya usimamizi mzuri wa rasilimali za umma na uwajibikaji kwa wananchi
Na Hagai Ruyagila
Mkuu wa mkoa wa Kigoma, Balozi Simon Sirro ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu kwa kupata hati safi kwa mwaka wa fedha unaoishia juni 2025, katika ukaguzi wa hesabu za serikali na ukusanyaji wa mapato ya ndani kwa asilimia 138, ikiwa ni halmashauri ya pili mkoani hapa kwa ukusanyaji wa mapato baada ya halmashauri ya wilaya ya Uvinza.
Balozi Sirro ametoa pongezi hizo wakati akizungumza katika mkutano maalum wa Baraza la Madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Kasulu, kilicholenga kujadili taarifa, hoja na mapendekezo ya mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali (CAG) kwa mwaka wa fedha 2024/2025.

Amesisitiza kuongeza ukusanyaji wa mapato na wakuu wa idara kutoa ushirikiano kwa wakaguzi ili kupunguza hoja zinazo andikwa na mkaguzi wa hesabu za serikali.
Mkuu wa Wilaya ya Kasulu, Kanali Isaac Mwakisu amewataka watumishi wa halmashauri ya wilaya ya Kasulu kufanya kazi kwa uwaminifu, ushirikiano na weledi katika utendaji wao wa kazi.

Mkaguzi Mkuu wa nje wa hesabu za serikali (CEA) Honest Muya amesisitiza kufanyia kazi mapendekezo yote yaliyotolewa na CAG kwa wakati ili kuimarisha uwajibikaji na uwazi kwa matumizi yenye tija.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Kasulu Mh Samweli Kadogo amewataka watumishi, viongozi na madiwani wa halmashauri hiyo kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu, bidii na uwajibikaji ili kuendeleza mafanikio yaliyopatikana halmashauri hiyo iendelee kupata hati safi wakati ujao.
