Joy FM
Joy FM
14 Aprili 2026, 12:41

Viongozi wa dini wana mchango mkubwa katika masuala ya ulinzi na usalama wa jamii kwani nafasi yao ina uzito kwa sababu wanaheshimiwa, wanaaminika, na wana uwezo wa kufikia watu wengi kwa urahisi.
Na Hagai Ruyagila
Viongozi wa dini katika Kata ya Nyamnyusi Wilayani Kasulu Mkoani Kigoma, wameaswa kuhubiri na kuhimiza matendo mema kwa waumini wao ili kujenga jamii yenye maadili mema na kudumisha amani.
Wito huo umetolewa na Mkaguzi msaidizi wa Polisi Willy Lupa ambaye ni Polisi Kata wa Kata ya Nyamnyusi, wakati akizungumza na wananchi wa kata hiyo.
Amesema Viongozi wa dini wana jukumu kubwa la kuwalea waumini wao katika misingi ya maadili mema, hali itakayosaidia kupunguza vitendo visivyofaa na kuimarisha ulinzi na usalama katika jamii.

Aidha, ameongeza kwa kuwasisitiza wananchi wa kata ya Nyamnyusi kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama kutoa ushahidi pale wanapohitajika, ili kusaidia hatua za kisheria kuchukuliwa dhidi ya wahalifu.
Baadhi ya viongozi wa dini wakiwakilishwa na Mchungaji Kiongozi wa Kanisa la Pentekoste Injili Tanzania, Mchungaji Jacob Isaac, amesema wataendelea kuhubiri amani na upendo.
