Joy FM

Majiko banifu yaleta afueni kwa kaya 1404 Uvinza

15 April 2026, 9:58 am

Mkuu wa Wilaya Uvinza Dinnah Mathamani akigawa majiko kwa wananchi, Piha na Mtandao

Majiko banifu ni aina ya majiko yaliyoboreshwa ili kutumia nishati kidogo na katika jamii nyingi, hasa vijijini, watu hutegemea kuni na mkaa kama vyanzo vikuu vya nishati ya kupikia kutokana na changamoto za kiafya, kiuchumi na kimazingira, matumizi ya majiko banifu yamekuwa suluhisho muhimu.

Na Mwandishi wetu

Wananchi wa Wilaya ya Uvinza wameanza kunufaika na mradi wa ugawaji majiko banifu 1,404 yanayotolewa kwa ruzuku ya Sh. 7,650, ikiwa ni sehemu ya juhudi za Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan katika kulinda afya ya jamii na kutunza mazingira.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa ugawaji huo, Mkuu wa Wilaya ya Uvinza, Mh.Dinah Mathamani amesema majiko hayo ni suluhisho muhimu kwa kaya nyingi za vijijini kwani yatapunguza matumizi ya kuni na mkaa, gharama za maisha na kuokoa muda wa kupika.

Mh. Dinah ameeleza kuwa wanawake watanufaika zaidi kwa kupata muda wa kushiriki shughuli za kiuchumi na kijamii badala ya kutumia muda mwingi jikoni.

Mkuu wa Wilaya ya Uvinza, Mh.Dinah Mathamani, Picha na Ofisi ya mawasiliano Uvinza

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza, CPA Fred Milanzi amesema Serikali imeendelea kuwaletea wananchi fursa na miradi yenye tija, na kwamba mradi huo utasaidia juhudi za uhifadhi wa mazingira kwa kupunguza ukataji miti ovyo kwa ajili ya kuni na mkaa ili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Wananchi wa Uvinza wameeleza kufurahishwa na mradi huo, wakisema utawapunguzia gharama za nishati, na kuahidi kuyatunza na kuyatumia ipasavyo ili kufanikisha malengo yaliyokusudiwa.

Wananchi wa Wilaya Uvinza wakiwa wamesubili kupewamajiko, Picha na Ofisi ya mawasiliano Uvinza

Kwa ujumla, mradi wa majiko banifu unatajwa kuwa kichocheo muhimu cha maendeleo ya kijamii na kiuchumi Uvinza, huku ukiendelea kuunga mkono dhamira ya serikali ya kuboresha maisha ya wananchi na kuhifadhi mazingira kwa vizazi vijavyo