Joy FM

Kigoma yaimarisha utayari wa kukabiliana na maafa

3 August 2026, 09:53

Baadhi ya wajumbe wakiwa kwenye kikao cha kuimarisha utayari wa kukabiliana na maafa Kigoma, Picha na Mwandishi wetu

Maafa ni matukio yanayosababisha madhara makubwa kwa watu, mali na mazingira na maafa yanaweza kuwa ya asili kama mafuriko, ukame, matetemeko ya ardhi na milipuko ya magonjwa, au yanayosababishwa na shughuli za binadamu kama moto na ajali

Na Mwandishi wetu

Serikali kupitia Wizara ya Afya na Ofisi ya Waziri Mkuu, Idara ya Menejimenti ya Maafa, kwa kushirikiana na CIHEB Tanzania chini ya Mradi wa Usalama wa Afya Duniani, imeendesha kikao cha Usimamizi Shirikishi kilichowakutanisha wataalamu wa afya na wadau kutoka sekta mbalimbali kwa lengo la kuandaa mikakati ya kuimarisha utayari wa kukabiliana na maafa na dharura katika Mkoa wa Kigoma.

Baadhi ya wajumbe wakiwa kwenye kikao cha kuimarisha utayari wa kukabiliana na maafa Kigoma, Picha na Mwandishi wetu

Kikao hicho kimefanyika leo, Julai 31, 2026, katika Kituo cha kuratibu operesheni za matukio ya dharura (PHEOC), kikilenga kupima na kutathmini utendaji wa sekta zinazohusika katika kukabiliana na maafa na milipuko ya magonjwa, ikiwemo mifumo ya mawasiliano, uratibu wa huduma na ushirikiano wa taasisi mbalimbali wakati wa dharura.

Akizungumza wakati wa kikao hicho, Dkt. Agnes Buchwa kutoka Kitengo cha dharura na maafa cha Wizara ya Afya amesema usimamizi shirikishi ni nguzo muhimu katika kuimarisha utayari wa Taifa wa kukabiliana na maafa na milipuko ya magonjwa, akisisitiza umuhimu wa uratibu madhubuti na ushirikiano kati ya sekta zote zinazohusika.

Dkt. Agnes Buchwa kutoka Kitengo cha Dharura na Maafa cha Wizara ya Afya, Picha na Mwandishi wetu

Naye, Mkurugenzi wa Ufundi wa CIHEB Tanzania, Siril Michael Kulaya, amesisitiza umuhimu wa ushirikiano wa sekta mbalimbali katika kuzuia, kujiandaa na kukabiliana na maafa na milipuko ya magonjwa ili kupunguza athari zinazoweza kujitokeza kwa jamii.