Joy FM
Joy FM
21 May 2026, 15:08

Elimu huwasaidia watoto kupata maarifa, maadili na stadi za maisha zinazowawezesha kujitegemea na kuwa na maisha bora ya sasa na ya baadaye na watoto wanaopata elimu huwa na nafasi kubwa ya kupata ajira, kupunguza umaskini na kuchangia maendeleo ya familia, jamii na taifa kwa ujumla
Na Hagai Ruyagila
Wazazi na Walezi Wilayani Buhigwe Mkoani Kigoma wameaswa kuwapeleka watoto wao shule ili wapate elimu itakayowasaidia katika maisha yao ya sasa na ya baadaye.
Wito huo umetolewa na Askofu wa Dayosisi ya Western Tanganyika Kanisa la Anglikana Tanzania, Mhashamu Emmanuel Charles Bwatta, wakati akiwawekea mikono wanafunzi wa darasa la kipaimara katika Kanisa la Anglikana Parishi na Dinari ya Mugera wilayani Buhigwe..

Askofu Bwatta amesema hayo baada ya baadhi ya wanafunzi waliohitimu darasa la kipaimara kutojua kusoma ndipo akasema elimu ni msingi muhimu kwa maendeleo ya mtoto, hivyo amemuagiza mchungaji wa kanisa hilo Mch. Laban Charles kuhakikisha watoto wanapata malezi bora ya kiroho pamoja na elimu itakayowajengea maisha yenye maadili mema.
Aidha, amewashauri wazazi kushirikiana na viongozi wa dini katika kuhakikisha watoto wanapata haki yao ya elimu.
Kwa upande wake, Mchungaji kiongozi wa Kanisa hilo, Ruldean Laban Charles, amesema kumlea mtoto kwenye misingi ya elimu ni jambo lenye tija maana unapomlea katika misingi ya dini itamsaidia kuwa na manufaa katika familia na taifa kwa ujumla.

Baadhi ya wazazi na walezi kutoka wilayani Buhigwe wamesema wanaendelea kuthamini mchango wa kanisa katika kuwalea watoto wao kiroho na kielimu, huku wakiahidi kushirikiana kuhakikisha watoto wanapata elimu bora kwa manufaa ya jamii na taifa kwa ujumla.
