Joy FM
Joy FM
12 May 2026, 09:48

Makanisa yana umuhimu mkubwa wa kuanzisha miradi ya kuongeza kipato kwa sababu yanasaidia kuimarisha huduma za kiroho na maendeleo ya jamii kwa ujumla
Na Hagai Ruyagila
Katika jitihada za kusaidia kupunguza tatizo la ukosefu wa ajira hapa nchini, Dayosisi ya Western Tanganyika Kanisa Anglikana Tanzania limenunua magari mawili aina ya Tata kwa ajili ya shughuli za usafirishaji wa abiria jambo ambalo kitasaidia baadhi ya vijana kupata ajira.

Akizungumza katika hafla ya kupokea magari hayo, Askofu Emmanuel Bwatta wa Dayosisi hiyo, amesema kuwa ununuzi wa magari hayo ni sehemu ya mikakati ya Dayosisi katika kuinua uchumi wa kanisa pamoja na kutoa fursa za ajira kwa vijana na wananchi wa eneo hilo.
Amesema kuwa magari hayo yatasaidia kuongeza mapato ya Dayosisi huku yakitoa huduma ya usafiri kwa wananchi, jambo ambalo litachochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika wilaya ya Kasulu na maeneo ya jirani.

Katibu Tawala wa Wilaya ya Kasulu Bi. Theresia Mtelewe, amepongeza Kanisa hilo kwa hatua hiyo akieleza kuwa uwekezaji huo utaongeza ajira na kuchangia ukuaji wa uchumi wa kanisa pamoja na taifa kwa ujumla kwani kanisa linakwenda kujitegemea.
Mwenyekiti wa Kamati ya Maendeleo wa kanisa la Anglikana Dayosisi ya Western Tanganyika, Ohadi Mdunya amesema ni vizuri kuwa na maoni yenye matokeo kama ambavyo askofu Bwatta anavyofanya ili kufanikisha miradi mingine ya maendeleo yenye lengo la kuimarisha uchumi wa kanisa.

Naye mwenyekiti wa maendeleo Kanisa kuu la Mt. Andrea Anglikana Kasulu Mjini Zabron Nashon amesema kuwa wana Fanya hivyo ili kutotegemea sadaka pekee bali kuanzisha miradi ambayo itasaidia Dayosisi hiyo kusonga mbele kiuchumi.