Joy FM

“Simamieni utekelezaji wa lishe na afya mama na mtoto” DC Buhigwe

8 May 2026, 16:54

Mkuu wa Wilaya Buhigwe akiwa na Mkurugenzi wa Wilaya hiyo na Katibu Tawala wa Wilaya Bi. Utefta Mahega, Picha na Ofisi ya Buhigwe dc

Lishe ni jambo muhimu sana katika maisha ya watoto kwa sababu huchangia ukuaji na maendeleo yao ya mwili na akili na mtoto anayepata lishe bora hukua vizuri, huwa na afya njema, na hupata nguvu za kufanya shughuli mbalimbali za kila siku

Na Mwandishi wetu

Mkuu wa Wilaya ya Buhigwe, Mhe. Kanali Michael Ngayalina amewataka watendaji na viongozi wa sekta mbalimbali Wilayani humo kuhakikisha wanafuatilia kwa karibu utekelezaji wa masuala ya lishe pamoja na kupiga vita mila na tamaduni potofu zinazochangia kudhoofisha afya ya mama na mtoto katika jamii.

Mkuu wa Wilaya ya Buhigwe, Mhe. Kanali Michael Ngayalina, Picha na Buhigwe Dc

Mhe. Kanali Ngayalina ambaye ndie mgeni rasmi katika kikao hicho, amesema hayo leo Mei 8, 2026 wakati wa kikao cha robo ya tatu cha Kamati ya Lishe ya Wilaya. Aidha, amempongeza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri kwa kutenga fedha kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli za lishe, akieleza kuwa hatua hiyo inaunga mkono Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050 inayolenga kuwa na jamii yenye afya bora.

Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Wilaya Bi. Utefta Mahega amewataka viongozi wa sekta ya afya kuhakikisha wanasimamia kikamilifu huduma za afya ya mama na mtoto, akieleza kuwa hatua hiyo itasaidia kujenga kizazi chenye afya na kuongeza ustawi wa jamii kwa ujumla.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Buhigwe Ndug. George Emmanuel Mbilinyi, ameahidi kusimamia na kutekeleza maazimio yote yaliyotolewa na Kamati ya Lishe, huku akisisitiza kuwa halmashauri itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha afua za lishe zinafikia malengo yaliyokusudiwa.

Baadhi ya viongozi wa Halmashauri ya Wilaya Buhigwe wakiwa katika kikao cha utekelezaji wa masuala ya lishe, Picha na Buhigwe Dc

Akiwasilisha taarifa ya hali ya lishe wilayani humo, Afisa Lishe Bi. Melina Jombe amesema wilaya imeendelea kupata mafanikio makubwa katika utekelezaji wa afua za lishe ambapo kiwango cha utekelezaji kimeongezeka kutoka asilimia 48 hadi asilimia 73, huku upatikanaji wa chakula shuleni ukifikia asilimia 99.1, hali inayochangia kuboresha afya na maendeleo ya wanafunzi.