Joy FM
Joy FM
14 Aprili 2026, 12:16

Kudhibiti kipindupindu kunategemea sana usafi, maji salama, na matibabu ya haraka na kuchukua hatua mapema ili kuokoa maisha ya watu.
Na Lucas Hoha
Mkoa wa Kigoma umefanikiwa kudhibiti mlipuko mpya wa ugonjwa wa kipindupindu ambao umekuwa ukisababishwa na mambo mbalimbali ikiwemo matumizi mabaya ya choo, uchafu na matumizi ya maji machafu katika Wilaya na Halmashauri za Mkoa wa Kigoma.
Hayo yamesemwa na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Damas Kayela wakati akifungua mafunzo yanayolenga kuwapatia Elimu wadau mbalimbali wa kudhibiti magonjwa ya mlipuko ikiwemo kipindupindu
Amesema tangu kutokea kwa mlipuko mwaka uliopita, Ofisi ya Mganga Mkuu wa Mkoa wakishirikiana na wadau wengine wamefanikiwa kudhibiti mlipuko wa ugonjwa huo licha ya uwepo wa mwingiliano wa watu kutoka mataifa jirani ikiwemo Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Magreth Mkude ni moja ya wadau kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Buhigwe amesema asilimia kubwa ya ugonjwa wa kipindupindu unatokana watu kushindwa kubadili tabia zao kwa kushindwa kutunza mazingira.

Kwa upande wake, Meneja wa Wakala wa Maji safi na Utunzaji wa Mazingira Vijijini RUWASA Mhandisi Alone Kaje amesema wananchi wanatakiwa kuendelea kupatiwa elimu ili kufahamu namna ya kujikinga na ugonjwa huo.
Mafunzo hayo ya Elimu ya kudhibiti mlipuko wa kipindupindu yamewakutanisha wadau mbalimbali wakiwemo viongozi kutoka Wizara ya Afya na Ofisi ya Rais Tamisemi yakilenga zaidi kuweka mikakati ya namna ya kukabiliana na kipindupindu kwenye jamii.