Joy FM

Madiwani waagiza utekelezaji wa miradi ya maendeleo Uvinza

29 April 2026, 08:50

Baadhi ya madiwani katika Halmashauri ya Wilaya Uvinza wakiwa katika baraza la madiwani, Picha na Ofisi ya mawasiliano Uvinza

Maendeleo ni msingi wa maisha bora na ustawi wa jamii yoyote bila maendeleo, ni vigumu kufikia malengo ya kijamii, kiuchumi na kisiasa

Na Mwandishi wetu

Baraza la kawaida la Madiwani Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza limeagiza utekelezaji wa miradi ya miundombinu ya maji, umeme na barabara inayodumu kwa muda mrefu kuharakishwa katika kata zenye changamoto, ili kuboresha upatikanaji wa huduma kwa wananchi.

Agizo hilo limetolewa leo, tarehe 28 Aprili, 2026 katika kikao cha Baraza la Madiwani kilichofanyika katika ukumbi wa Halmashauri, ambapo kata zilizotajwa kuwa na changamoto ni Mwakizenga, Kalya, Sunuka na Sigunga.

Katika kikao hicho, wajumbe walijadili taarifa ya utekelezaji wa shughuli za kata kwa robo ya tatu ya mwaka wa fedha 2025/2026, wakisisitiza umuhimu wa kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Baadhi ya madiwani katika Halmashauri ya Wilaya Uvinza wakiwa katika baraza la madiwani, Picha na Ofisi ya mawasiliano Uvinza

Akizungumza wakati wa kikao hicho, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza, Mh. Salvatory Motto, aliwataka watendaji kusikiliza wananchi kwa makini na kuwahudumia kwa upendo, ili kutatua changamoto zinazowakabili kwa wakati.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Uvinza, Mh. Dinah Mathamani, aliwahimiza wajumbe kushirikiana kwa umoja na mshikamano katika kusukuma mbele agenda za maendeleo ya Halmashauri, kwa manufaa ya wananchi wote.

Mkuu wa Wilaya ya Uvinza Mh. Dinah Mathamani Picha na Ofisi ya mawasiliano Uvinza