Joy FM

DC Kasulu ataka wananchi kuepuka vitendo vya uvunjifu wa amani

6 July 2026, 09:09

Mkuu wa Wilaya Kasulu Kanal Isaac Mwakisu akiwa na viongozi wengine, Picha na Mwandishi wetu

Amani ni hali ya utulivu, usalama na maelewano miongoni mwa watu katika jamii ni msingi muhimu unaowezesha wananchi kuishi kwa upendo, kufanya shughuli zao za kila siku na kushiriki katika maendeleo ya taifa

Na Mwandishi wetu

Mkuu wa Wilaya ya Kasulu, Mhe. Kanali Isaack Mwakisu, amesema kuwa amani ndiyo nguzo kuu ya ustawi wa jamii na maendeleo ya taifa lolote, akionya kuwa uvunjifu wa amani unaweza kuhatarisha usalama wa wananchi pamoja na maendeleo ya nchi.

Kanali Mwakisu ametoa kauli hiyo leo, Ijumaa, Julai 3, 2026, wakati Kamati ya Usalama ya Wilaya ilipofanya ziara ya kukagua miradi inayotarajiwa kutembelewa na Mwenge wa Uhuru 2026 katika Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu.

Akizungumza katika ziara hiyo, amesema kumekuwa na wito unaosambaa kupitia mitandao ya kijamii unaohamasisha wananchi kuandamana tarehe Julai 7 badala ya kushiriki maadhimisho ya sikukuu ya kitaifa, na kuwataka wananchi kuepuka kushiriki vitendo vinavyoweza kuhatarisha amani.

Mkuu wa Wilaya Kasulu Kanal Isaac Mwakisu akiwa na viongozi wengine, Picha na Mwandishi wetu

“Nawasihi mjiepushe kabisa na hamasa hiyo, kwa kuwa amani yetu ndiyo maendeleo yetu, amani yetu ndiyo usalama wetu, na amani yetu ndiyo msingi wa ustawi wa jamii pamoja na maendeleo ya taifa. Hivyo, ni wajibu wetu sote kuitunza,” amesema Kanali Mwakisu.

Aidha, Mkuu huyo wa Wilaya amewataka wananchi kuchukua tahadhari dhidi ya mvua kubwa zinazotarajiwa kunyesha, ambazo zinaweza kusababisha mafuriko na kuharibu miundombinu. Amesisitiza umuhimu wa kuzingatia ushauri wa wataalamu na kuchukua hatua za kujikinga ili kuepusha madhara yanayoweza kujitokeza.

Mkuu wa Wilaya Kasulu Kanal Isaac Mwakisu akiwa na viongozi wengine, Picha na Mwandishi wetu

Katika ziara hiyo, Kamati ya Usalama ilikagua miradi mbalimbali itakayopitiwa na Mwenge wa Uhuru 2026, ikiwemo ujenzi wa madarasa mawili katika Shule ya Sekondari Nyamidaho, mradi wa Umoja wa Madereva Makere, Kituo cha Kujaza Mafuta Nyachenda, ujenzi na upanuzi wa Zahanati ya Kitema, pamoja na Mradi wa Maji Chekenya.