Joy FM
Joy FM
8 July 2026, 17:13

Ushiriki wa wananchi katika shughuli za maendeleo ni msingi muhimu wa kujenga jamii yenye maendeleo endelevu na miongoni mwa shughuli hizo ni kujitolea kushiriki katika ujenzi na matengenezo ya barabara, madaraja, shule na vituo vya afya
Na Hagai Ruyagila
Wakazi wa Mtaa wa Boma, Kata ya Kimobwa katika Halmashauri ya Mji Kasulu mkoani Kigoma, wamejitolea kushiriki katika ujenzi na matengenezo ya barabara ya mtaa wao kwa lengo la kuboresha miundombinu na kuwezesha shughuli za maendeleo pamoja na huduma mbalimbali kuwafikia wananchi kwa urahisi
Akizungumza na wakazi hao muda mfupi baada ya kufanyika kwa zoezi la matengenezo ya Barabara Mwenyekiti wa Mtaa wa Boma Majariwa Biseka Bisoze amesema ushirikiano ulioonyeshwa na wananchi ni mfano wa uzalendo na mshikamano unaopaswa kuigwa na jamii katika kutatua changamoto zinazowakabili.

Amesema matengenezo ya Barabara hiyo yanalenga kusogeza huduma karibu na Wananchi kutokana na baadhi ya wakazi wa mtaa huo kukosa Barabara inayowaunganisha na maeneo mengine
Wakizungumza baada ya kukamilisha hatua ya kwanza ya zoezi hilo la kujitolea, wamesema wameamua kuunganisha nguvu zao ili kuhakikisha barabara hiyo inapitika wakati wote na kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika eneo lao.

Naye Afisa Mtendaji wa Mtaa wa Boma, Bi. Hekima Barosha, amesema ofisi ya mtaa kwa kushirikiana ofisi ya kata watawasikiana na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) ili kuendelea na hatua zinazofuata za kuboresha barabara hiyo kwa kiwango kinachostahili.

Hatua ya pili ya wananchi hao kutengeneza barabara hiyo inatarajiwa kuendelea jumatano ya wiki ijayo mnamo tarehe 15 mwezi julai 2026