Joy FM
Joy FM
7 July 2025, 12:59

Vikundi vya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu wametakiwa kutumia mikopo inayotolewa na Halmashauri kutumia mikopo hiyo kwa malengo yaliyokusudiwa.
Na Mwandishi
Zaidi ya shilingi milioni 800 zinatarajia kutolewa na Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma kwa vikundi 71 vya wajasiliamali na wafanyabiashara wadogo ili waweze kukuza na kuinua biashara zao.
Mkuu wa Wilaya Kigoma, Dk. Rashid Chuachua amesema hayo wakati benki ya CRDB kupitia program ya utoaji mikopo ya asilimia 10 kutumia mfumo jumuishi (iMBEJU) inayosimamiwa na CRDB Foundation ikikabidhi kiasi cha shilingi milioni 63.5 kwa vikundi nane vya wajasiliamali wa manispaa ya Kigoma Ujiji.
Katika hotuba iliyotolewa kwa niaba yake na Katibu Tawala wa wilaya Kigoma, Mganwa Nzota amesema kuwa mikopo hiyo inatolewa kuwezesha idadi kubwa ya wananchi wa Manispaa ya Kigoma Ujiji kufanya biashara zao kwa tija kubwa ili kuimarisha uchumi wa familia zao.
Dk. Chuachua amesema kuwa mikopo hiyo ambayo haina riba inalenga kuwaondoa watu wa makundi maalum kwenye changamoto ya kuchukua mikopo yenye riba kwenye taasisi binafasi zinazotoa mikopo ambazo pamoja na kuwa na riba kubwa ambazo zimesababisha wajasilimali kurudisha mikopo lakini pia mali na bidhaa zao zimekuwa zikikamatwa na kutaifishwa na taasisi.
Akizungumza katika utoaji mikopo hiyo Meneja wa CRDB Bank Foundation, Fadhili Bushagama amesema kuwa vikundi nane vinapatiwa mikopo hiyo yenye thamani ya shilingi milioni 63.5 baada ya kukidhi vigezo na michakato mbalimbali iliyofanyika kutafuta vikundi hivyo.
Bushagama amesema kuwa katika mchakato huo vikundi 18 vilitembelewa kufanyiwa mchakato wa kujua uendeshaji wa biashara zao, utunzaji wa hesabu, taratibu nzuri za utunzaji wa fedha na taratibu nzuri za taarifa ya biashara na hivyo kufanikiwa kupata mikopo hiyo na kwamba vikundi 98 viliainishwa awali vikiomba mkopo.