Joy FM
Joy FM
7 May 2026, 09:39

Mapato ya halmashauri ni msingi muhimu wa maendeleo ya jamii na utoaji wa huduma za kijamii kama vile elimu, afya, maji, na miundombinu, Halmashauri hukusanya mapato kupitia ushuru, ada mbalimbali, na tozo zinazolipwa na wananchi pamoja na wafanyabiashara.
Na Dotto Josephati
Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Kibondo limeagiza watendaji wote wa kata kusimamia kikamilifu mawakala wanaokusanya mapato ya halmashauri kwa kuhakikisha wanatumia mfumo wa kielektroniki (TOS), hatua inayolenga kuongeza uwazi, ufanisi na kudhibiti upotevu wa mapato.
Maagizo hayo yametolewa na Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Mh. Alex Sylvester Baragomwa, kwa niaba ya baraza hilo, wakati wa kikao cha Baraza la Madiwani cha robo ya tatu ya mwaka wa fedha 2025/2026, kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa IOM.

Mwenyekiti huyo amesema kuwa ukusanyaji wa mapato ni ajenda ya kudumu ya halmashauri, hivyo matumizi ya mfumo wa kielektroniki kwa mawakala yataziba mianya ya ubadhirifu na kuongeza uaminifu kwa wananchi wanaolipa tozo mbalimbali.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibondo, Stephen Janks, amewataka wajumbe wa baraza hilo kutoa elimu kwa wazazi kuhusu mkakati mahsusi wa kuboresha ufaulu wa wanafunzi na kuwa mkakati huo unalenga kuimarisha mbinu bora za kujifunza, ikiwemo matumizi sahihi ya mbinu ya kukariri sambamba na kuelewa wanachojifunza katika masomo ya shule za msingi na sekondari.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kibondo, Aggrey Mwagaza, amewataka madiwani kuacha mivutano ya kisiasa isiyo na tija na badala yake kuzingatia maslahi ya wananchi kwa kushirikiana na wataalam katika kufanya maamuzi sahihi ya maendeleo.