Joy FM

Timu ya kutathimini mikopo yakagua miradi ya vikundi Uvinza

13 June 2026, 13:16

Ni timu ya kutathimini miradi ya vikundi ikiwa imetembelea vikundi, Picha na Uvinza DC

Wakati vikundi mbalimbali vilivyokidhi vigezo na kupokea mikopo vikiwa vinaendelea utekelezaji wa miradi yao timu ya kutathimini mikopo imewatembelea ili kujionea shughuli wanazofanya

Na Mwandishi wetu

Timu ya tathmini ya vikundi ngazi ya Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza imetembelea vikundi vitano vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu katika Kata za Itebula na Mwakizega kwa lengo la kuhakiki hali halisi ya miradi iliyoomba mikopo ya asilimia 10 kabla ya hatua za utoaji wa fedha.

Muonekano wa kuku wakiwa kwenye banda ambao wanamilikiwa na kikundi, Picha na Uvinza DC

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mwenyekiti wa timu ya tathmini, Godfrid Nkuba, amewasihi wanavikundi kusimamia na kuendesha miradi yao kwa bidii, uwajibikaji na kujituma ili kufanikisha malengo waliyojiwekea, kuongeza kipato chao na kuchangia maendeleo ya jamii kwa ujumla.

Aidha, wajumbe wa timu hiyo wamewataka wanavikundi kuendelea kushirikiana na kudumisha umoja katika utekelezaji wa shughuli zao, huku wakishirikisha viongozi na wataalamu wa halmashauri wanapokumbana na changamoto mbalimbali ili zipatiwe ufumbuzi kwa wakati na kuhakikisha miradi inakuwa endelevu na yenye manufaa kwa wanachama wote.

Ng’ombe wanaomilikiwa na kikundi picha na Uvinza DC

Timu hiyo iliyojumuisha wataalamu kutoka idara na vitengo mbalimbali ikiwemo Fedha na Biashara, Kilimo na Mifugo, Ushirika pamoja na Maendeleo na Ustawi wa Jamii, ilitoa ushauri wa kitaalamu kwa vikundi vilivyotembelewa kuhusu namna bora ya kuimarisha usimamizi wa miradi, matumizi sahihi ya rasilimali na uwekaji wa kumbukumbu za shughuli za kiuchumi.

Kikundi cha akinamama wafuma mashuka, Picha na Uvinza DC

Ushauri huo unalenga kuongeza ufanisi, tija na kuhakikisha miradi hiyo inakuwa endelevu na kuleta manufaa kwa wanachama pamoja na jamii inayowazunguka.