Joy FM
Joy FM
7 July 2026, 12:46

Kuimarisha ulinzi na usalama husaidia kulinda maisha ya wananchi na mali zao na hali hii huwafanya wananchi kuishi na kufanya shughuli zao bila hofu.
Na Orida Sayon
Jeshi la Polisi Mkoa wa Kigoma limesema limejipanga kikamilifu kuhakikisha ulinzi na usalama wa raia pamoja na mali zao kwa kuendelea kudhibiti matukio ya uhalifu katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo.
Akizungumza na kituo hiki, Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Kigoma, SACP Filemoni Makungu, amesema ushirikiano mzuri kati ya Jeshi la Polisi na wananchi umeendelea kuzaa matunda kwa kusaidia kudhibiti matukio mbalimbali ya kihalifu.
Amesema kuongezeka kwa uelewa wa wananchi kuhusu dhana ya Polisi Jamii kumesaidia kuimarisha ushirikiano na kuondoa hofu iliyokuwepo hapo awali.
Aidha Kamanda Makungu pia amewatoa hofu wananchi wa Mkoa wa Kigoma wakati wa maadhimisho ya Sikukuu ya Sabasaba, akiwataka kuendelea na shughuli zao za kila siku kwa amani, huku akibainisha kuwa Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama kuimarisha doria katika maeneo mbalimbali ili kuhakikisha amani na utulivu vinaendelea kudumishwa.
Aidha, ametoa wito kwa wananchi kuendelea kutii sheria bila shuruti, kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama, na kutoa taarifa kwa wakati kuhusu viashiria au matukio yoyote yanayoweza kuhatarisha amani katika maeneo yao.