Joy FM
Joy FM
5 August 2026, 09:59

Watumishi wa Mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira Manispaa ya Kigoma Ujiji KUWASA wametakiwa kuharakisha zoezi la kubaini, kuondoa na kudhibiti miundombinu ya zamani inayopitisha maji katika maeneo mbalimbali ya wananchi
Na Mwandishi wetu
Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Kigoma (KUWASA), Dkt. Christopher Nditi, amefanya kikao na Idara ya Ufundi na Uzalishaji Maji kwa lengo la kujadili na kuweka mikakati ya kudhibiti miundombinu ya maji katika eneo la Bwawa la Katubuka.
Katika kikao hicho, Dkt. Nditi ameagiza kazi ya kuondoa na kudhibiti miundombinu inayopitisha au kupeleka maji katika eneo hilo, ambalo awali lilikuwa makazi ya wananchi, ifanyike kwa haraka. Amesema hatua hiyo italenga kuokoa maji yanayoweza kuwa yanapotea kutokana na uvujaji wa miundombinu, hali inayodhaniwa kuchangia eneo hilo kuendelea kuwa na maji kwa takribani miaka mitano tangu lilipojaa maji mwaka 2022.

Aidha, Dkt. Nditi amewataka mafundi na wataalamu wa KUWASA kuimarisha ushirikiano wanapokabiliana na changamoto zinazohusisha miundombinu ya maji. Amesisitiza kuwa masuala ya kitaalamu yanapaswa kushughulikiwa na jopo la wataalamu kwa pamoja ili kupata suluhisho la haraka na lenye tija, badala ya kuyaachia watu wachache.
Akizungumza katika kikao hicho, Kaimu Mkurugenzi wa Uzalishaji na Usambazaji Maji, Mhandisi Francisco Makoye, amesema utekelezaji wa awali tayari umeanza. Ameeleza kuwa wataalamu wamefanikiwa kubaini baadhi ya Bomba kubwa zilizopi katika eneo hilo na kwamba kazi ya kudhibiti inaendelea vizuri, huku ikitarajiwa kukamilika ndani ya muda mfupi.