Joy FM
Joy FM
2 October 2026, 12:59

Wakala wa vipomo WMA Mkoani Kigoma umesema utawachukulia sheria mawakala ambao wamekuwa wakijaza mitungi ya gesi pungufu huku wakiwataka wanannchi kupima mitungi hiyo kabla ya kujaza
Na Josephine Kiravu
Wananchi mkoani Kigoma wametakiwa kuhakikisha wanapima ujazo wa mitungi ya gesi wanapofika kwa mawakala kwa ajili ya kubadilisha mitungi hiyo, hatua inayolenga kuondoa changamoto na malalamiko ya kupungua kwa ujazo wa gesi.
Wito huo umetolewa wakati wa ukaguzi wa ujazo wa mitungi ya gesi uliofanyika katika baadhi ya vituo vya kubadilisha mitungi mkoani Kigoma, ambapo baadhi ya mawakala walibainika kutokuwa na mizani kwa ajili ya kupimia ujazo wa gesi.
Katika ukaguzi huo, pia mtungi mmoja ulibainika kuwa haukuwa umefikia ujazo uliotakiwa.

Akizungumza baada ya kufanya ukaguzi huo, Meneja wa Wakala wa Vipimo Mkoa wa Kigoma, Laurent Kabikiye, amewataka mawakala wanaojihusisha na kubadilisha na kuuza mitungi ya gesi kuhakikisha wanakuwa na mizani inayokidhi mahitaji ili kuwawezesha kupima ujazo wa gesi na kuepuka kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.
Kabikiye amesema uwepo wa mizani katika vituo vya kubadilisha mitungi ni muhimu kwa ajili ya kuhakikisha wananchi wanapata ujazo unaostahili na pia kupunguza malalamiko yanayoweza kujitokeza.

Kwa upande wake, Wakala Mkuu wa Oryx mkoani Kigoma, Issa Mangapi, amewataka wananchi kufuata maelekezo wanayopewa wanapofika katika vituo vya kubadilisha mitungi ya gesi.
Mangapi amesisitiza umuhimu wa wananchi kuhakikisha wanapima ujazo wa mtungi kabla ya kuuchukua na kwenda nao nyumbani, ili kujiridhisha kuwa wamepata ujazo unaotakiwa.
Hatua hiyo inalenga kuongeza uelewa kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kupima ujazo wa mitungi ya gesi na kuhakikisha wafanyabiashara wanazingatia viwango vinavyotakiwa.