Joy FM
Joy FM
19 October 2026, 12:55

Hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Kigoma Maweni imeanzia kambi ya matibabu ya kibingwa na bobezi kwa wananchi
Na Timotheo Leonard
Zaidi ya wananchi 3,500 wanatarajiwa kunufaika na huduma za matibabu ya kibingwa na bingwa bobezi kupitia kambi maalumu itakayofanyika katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kigoma Maweni kuanzia Oktoba 19 hadi 23, mwaka huu.
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari Mganga mfawidhi Hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Kigoma Maweni Dr. Joseph Nangawe, amesema Kambi hiyo ya siku tano inalenga kutoa huduma za matibabu na uchunguzi wa magonjwa mbalimbali, ikiwemo magonjwa yanayohitaji upasuaji, matatizo ya macho, masikio, pua na koo, pamoja na uchunguzi wa magonjwa kwa kutumia mionzi.
Dr.Nangawe anasema lengo la Serikali ya awamu ya sita kusogeza huduma hiyo ya matibabu ya kibingwa ni kuwapunguzia gharama wananchi kwenda katika hospitali za kanda kutafuta matibabu.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya kambi hiyo, Dkt. Ashraf Bitaliho, anasema huduma hizo zitatolewa kwa wagonjwa wenye bima za afya na wale wasio na bima, huku akiwahimiza wananchi wote wa Mkoa wa Kigoma kujitokeza kupata huduma hizo.