Joy FM

Wavamizi watakiwa kupisha kitalu cha uwindaji Uvinza -Makere

19 October 2026, 08:56

Mkuu wa Mkoa wa Kigoma akiwa katika mkutano wa hadhara na wananchi, Picha na Mwandishi wetu

Jumla ya kaya 452 bado zinaendelea kuishi katika Kitalu hicho kilichopo katika wilaya za Kasulu na Uvinza baada ya kutekelezwa kwa agizo la awali la wavamizi hao kuhamia eneo lililotengwa na Serikali kwenye Kitongoji cha Katoto, kata ya Kagerankanda Wilayani Kasulu.

Na Mwandishi wetu

Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Balozi Simon Sirro amewataka wavamizi wanaoendelea kuishi katika Kitalu cha Uwindaji wa kitalii cha Uvinza-Makere, kupisha eneo hilo ili kuruhusu matumizi yaliyopangwa na serikali.

Akizungumza na wananchi hao, Balozi Sirro amesema baadhi yao hawakuwa wakiishi eneo hilo wakati serikali ikiwahamishia wenzao kwenye kitongoji cha Katoto huku akiwataka kujiorodhesha kwenye Mamlaka husika ili kupangiwa maeneo mengine ya kuishi.

Baadhi wa wananchi wakiwa kwenye mkutano wa hadhara, Puicha na Mwandishi wetu

Naye Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu Mbelekwa Vanika amesema, dai la wavamizi hao la uwepo wa kitongoji cha Katoto B wanachoishi sasa, halina uhalali kwani hakuna utambuzi rasmi wa eneo hilo ndani ya Kitalu hicho.

Amesema Serikali ilishatenga Hekta 4,446 kutoka eneo la hifadhi ya kitalu na kuzijumuisha katika kitongoji cha Katoto kwa ajili ya makazi, mashamba, ufugaji na taasisi za kutolea huduma, kwa jumla ya kaya 1200 zilizotambuliwa zikiishi katika hifadhi hiyo hapo awali.

Mkuu wa Mkoa wa Kigoma akiwa katika mkutano wa hadhara na wananchi, Picha na Mwandishi wetu

Upande wake, Mwenyekiti wa Kijiji cha Kagerankanda Helman Mtibilo amesema jumla ya wakazi 1200 waliotengewa eneo la kuishi katika kitongoji cha Katoto wamepatiwa maeneo yao na hakuna aliyekosa.

Aidha, amesema anashangazwa na kitendo cha kuibuka kwa kundi hilo linalodai kutotambuliwa wakati wa zoezi la kutenga makazi kwa waliobainika kuishi ndani ya eneo la Kitalu hicho.