Joy FM
Joy FM
7 November 2026, 22:50

Halmashauri ya Wilaya Uvinza Mkaoni Kigoma imezindua rasmi msimu wa kilimo wa mwaka 2026/2027 ambapo wakulima wameaswa kuzingatia kanuni bora za kilimo ili waweze kupata mazao mengi yenye tija na kuachana na kilimo cha mazoea
Na Mwandishi wetu
Mkuu wa Wilaya ya Uvinza Mkoani Kigoma Mh. Mtella Allam Mwampamba, amewataka wakulima Wilayani humo kuachana na kilimo cha mazoea na badala yake wajikite katika kilimo cha biashara kinachozingatia kanuni bora za kilimo ili kuongeza uzalishaji na kipato cha kaya.

Akizungumza wakati wa uzinduzi rasmi wa msimu mpya wa kilimo wa mwaka 2026/2027 Mwampamba amesema wakulima wanapaswa kutumia mbinu za kisasa za kilimo, kuzingatia ushauri wa wataalamu pamoja na kufuata kanuni bora za uzalishaji ili kuhakikisha kilimo kinakuwa shughuli yenye tija na inayochangia maendeleo ya kiuchumi.
Aidha, amewataka maafisa ugani na wataalamu wa kilimo kuacha utaratibu wa kukaa ofisini na badala yake kuwafikia wakulima katika maeneo yao ya uzalishaji ili kuwapatia elimu na ushauri wa kitaalamu utakaowasaidia kuongeza tija katika kilimo.

Naye Afisa Kilimo wa Wilaya ya Uvinza, Atoligwe Kaisi, amewahimiza wakulima kutumia mbolea kwa kuzingatia maelekezo ya kitaalamu ili kuboresha rutuba ya udongo na kuongeza uzalishaji wa mazao.
Amesema wilaya hiyo inalenga zaidi kuongeza uzalishaji wa mazao kwa kufikia zaidi ya tani milioni moja, hatua inayohitaji ushiriki wa wakulima katika kutumia pembejeo na teknolojia sahihi za kilimo.

Baadhi ya wakulima wa Wilaya ya Uvinza wameeleza kuwa wamepokea maelekezo hayo na kuahidi kuzingatia kanuni bora za kilimo cha biashara ili kuongeza mavuno, kipato na kunufaika zaidi na shughuli za kilimo.
Wamesema wamekuwa wakifanya kilimo cha mazoea ambacho hakijawapa tija inayotarajiwa, hivyo msimu huu wamejipanga kubadilika kwa kufuata ushauri wa wataalamu na kutumia mbinu bora za uzalishaji.
