Joy FM
Joy FM
22 October 2026, 11:03

Ujenzi wa shule ni muhimu kwa maendeleo ya watoto
Na Hagai Ruyagila
Zaidi ya shilingi milioni 100 zinahitajika kwa ajili ya kulipa fidia kwa wananchi wa Kata ya Mwilamvya, Halmashauri ya Mji wa Kasulu Mkoani Kigoma, waliopisha maeneo yao kwa ajili ya ujenzi wa shule mpya ya msingi.
Akizungumza kuhusu suala hilo, Kaimu Afisa Mtendaji wa Kata ya Mwilamvya, Iddy Emmanuel, amesema mchakato wa kufanya uthamini wa maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya ujenzi wa shule hiyo umekamilika.
Amesema hatua inayofuata ni kufanya mazungumzo na wananchi kuhusu namna ya kuchangia fedha zitakazosaidia kufanikisha ujenzi wa shule hiyo.

Kwa mujibu wa Emmanuel, ongezeko la idadi ya wanafunzi katika kata hiyo limeongeza uhitaji wa kuwa na shule nyingine ya msingi, kwani kwa sasa kata hiyo ina shule moja tu ya msingi ya serikali.
Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Mwilamvya, Emmanuel Gamuye, amewahimiza wananchi kuweka kipaumbele katika kuchangia shughuli za maendeleo ili kuharakisha utekelezaji wa miradi inayolenga kuboresha huduma katika kata hiyo.
Gamuye ameeleza kuwa wananchi wanapaswa kuelekeza nguvu na rasilimali zaidi katika shughuli za maendeleo badala ya kutumia sehemu kubwa ya rasilimali zao katika sherehe za harusi.

Naye, baadhi ya wananchi wa Kata ya Mwilamvya wamesema ongezeko la idadi ya watoto limekuwa miongoni mwa sababu zilizowasukuma kushirikiana na viongozi kuanzisha mchakato wa ujenzi wa shule mpya ya msingi.
Wamesema ujenzi wa shule hiyo unalenga kukidhi mahitaji ya elimu yanayotokana na ongezeko la watoto katika kata hiyo.