Joy FM
Joy FM
28 November 2026, 19:22

JMAT ni jumuiya ya amani na maridhiano iliayoanzishwa ili kuwaleta pamoja viongozi wa dini mbalimbali na jamii kwa ujumla ili kulinda, kudumisha na kuimarisha amani, umoja, mshikamano na maridhiano nchini Tanzania.
Na Tryphone Odace
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Amani na Maridhiano Tanzania, Sheikh Profesa Alhad Mussa Salum, ametoa wito kwa viongozi wa dini na wananchi kuendelea kudumisha umoja, mshikamano na kuishi kwa amani ili kuimarisha misingi ya utulivu na maridhiano nchini.

Sheikh Profesa Salum ametoa wito huo wakati wa ziara yake katika Wilaya za Kigoma na Kasulu mkoani Kigoma, ambapo amekutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa dini mbalimbali kwa lengo la kuhamasisha mshikamano, maelewano na ushirikiano miongoni mwa wananchi bila kujali tofauti zao za kiimani.
Akizungumza katika ziara hiyo, amesisitiza umuhimu wa viongozi wa dini kutumia nafasi zao kuelimisha jamii kuhusu upendo, kuvumiliana na kuepuka vitendo vinavyoweza kuvuruga amani na mshikamano wa kitaifa.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kasulu, Luteni Kanali Joseph Murimi, amesema Jumuiya ya amani na Maridhiano imekuwa chombo muhimu katika kuwaleta pamoja wananchi wa makundi mbalimbali na kuimarisha mahusiano yao katika jamii.
Amesema uwepo wa jumuiya hiyo una nafasi kubwa katika kuhamasisha mazungumzo, kujenga uelewano na kuzuia migogoro inayoweza kuathiri amani na maendeleo ya wananchi.

Baadhi ya viongozi wa dini walioshiriki katika mikutano hiyo wameipongeza jumuiya hiyo kwa mchango wake katika kuimarisha amani nchini, wakieleza kuwa imeendelea kuwa nguvu muhimu katika kuunganisha jamii na kuhimiza watu wenye mitazamo na imani tofauti kuishi kwa kuheshimiana.

Wamesema ushirikiano kati ya viongozi wa dini, serikali na wananchi ni muhimu katika kulinda amani iliyopo na kuhakikisha inaendelea kuwa msingi wa maendeleo ya taifa.
