Joy FM
Joy FM
2 November 2026, 18:56

Wananchi na familia zilizoathirika na mvua Mkoani Kigoma wametakiwa kuendelea kuchukua tahadhali ya mvua kipindi hiki ambacho mvua zinaendelea kunyesha
Na Mwandishi wetu
Jumla ya nyumba 121 na makanisa manne zimeezuliwa paa, huku nyingine zikiharibika kufuatia mvua kubwa zinazoendelea kunyesha katika Manispaa ya Kigoma Ujiji, ambapo kwa kipindi cha mwezi mmoja tangu kuanza kwa mvua hizo, zaidi ya kaya 100 zimeathirika.
Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Kigoma Ujiji, Hashim Mvogogo, ametoa taarifa hiyo wakati akimweleza Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Balozi Simon Sirro, ambaye aliongoza Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa pamoja na Kamati ya Maafa kukabidhi misaada iliyotolewa na halmashauri kwa waathirika wa mvua hizo.

Mvogogo amesema kata zilizoathirika zaidi ni Gungu, ambako nyumba 70 zimeathirika, Kibirizi nyumba 47, Mwanga Kusini nyumba mbili na Katubuka nyumba mbili.

Amesema katika kukabiliana na hali hiyo, halmashauri imewasilisha tani 2.6 za mchele, tani 1.9 za unga wa mahindi, tani moja ya maharage pamoja na sukari, mafuta ya kupikia na sabuni za kufulia