Joy FM
Joy FM
20 November 2026, 13:54

Utekelezaji wa miradi hiyo ni sehemu ya mikakati ya kusogeza na kuboresha utoaji huduma za wananchi
Na Mwandishi wetu
Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko imeendelea kuimarisha usimamizi na ufuatiliaji wa miradi ya maendeleo ili kuhakikisha inatekelezwa kwa ubora, ufanisi na kwa wakati, na kuongeza tija katika matumizi ya fedha za umma na utoaji wa huduma kwa wananchi.
Katika hatua hiyo, Kamati ya tathmini na ufuatiliaji ya Halmashauri, ikiongozwa na Mwenyekiti wake, Festo Basugoya, imefanya ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa Shule ya Msingi Kivuruga, iliyopo Kijiji cha Kabale, Kata ya Gwarama, pamoja na ujenzi wa nyumba za wakuu wa idara wilayani humo.Ziara hiyo iliyofanyika jana Alhamisi, Novemba 19, 2026, imelenga kutathmini maendeleo ya miradi, kubaini changamoto zinazoweza kuchelewesha ukamilishaji wake na kuhakikisha kazi zinafanyika kwa kuzingatia mikataba na viwango vya ubora vinavyotakiwa.

Akizungumza wakati wa ukaguzi huo, Mwenyekiti wa Kamati, Ndugu Festo Basugoya, amewataka wakandarasi kuongeza kasi ya utekelezaji wa kazi, kuzingatia ubora na kukamilisha miradi ndani ya muda uliopangwa, akisisitiza kuwa ucheleweshaji unaathiri wananchi wanaotarajia kunufaika na huduma hizo.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa usimamizi wa karibu, uwajibikaji na nidhamu katika utekelezaji wa miradi ili kuhakikisha fedha za maendeleo zinatumika kwa tija na kuleta matokeo yaliyokusudiwa.

Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko kupitia kamati zake inaendelea kusimamia na kufuatilia miradi ya maendeleo ili kuhakikisha inakamilika kwa wakati, kwa viwango vinavyotakiwa na kuimarisha upatikanaji wa huduma bora kwa wananchi.