Joy FM

Wakulima Kigoma waaswa kuzingitia kilimo bora

19 October 2026, 16:32

Baadhi ya wakulima wa Mkoa wa kigoma wakiwa katika semina ya kulimo, Picha na Sadick Kibwana

Benki ya Kilimo TADB imewataka wakulima Mkoani Kigoma kuzingatia kilimo bora ili kuhakikisha wanapata mazao yenye ushindani katika soko la ndani na nje

Na Sadick Kibwana

Wakulima Mkoani Kigoma wameaswa kuwa na mtazamo wa kuendesha kilimo cha kibiashara kwa kuzingatia mbinu bora na uchaguzi sahihi wa mazao yenye soko la uhakika.

Rai hiyo imetolewa na Afisa Maendeleo ya Biashara kutoka Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania – TADB Makao Makuu, Bi Angelina Nyansambo, wakati wa mafunzo ya siku mbili yaliyowakutanisha zaidi ya washiriki 100 kutoka vikundi mbalimbali vya wakulima Wilayani Kigoma.

Afisa Maendeleo ya Biashara kutoka Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania – TADB Makao Makuu, Bi Angelina Nyansambo, Picha na Sadick Kibwana

Bi Angelina amesema ili kuwa na kilimo chenye tija, ni lazima mkulima atumie mbinu zitakazovutia soko na wateja.

Naye Afisa Maendeleo ya Biashara wa Benki ya TADB Mkoa wa Kigoma, Bw. Patrick D. Kapungu, amesema lengo la semina hiyo ni kuwawezesha wakulima kupata elimu na matumizi sahihi ya mikopo inayotolewa na benki hiyo.

Kwa upande wao, baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo wamesema ujuzi na mbinu walizopatiwa ni bora na wana imani zitawasaidia kuongeza uzalishaji na kipato.

Baadhi ya wakulima, Picha na Sadick Kibwana

TADB imeendesha mafunzo hayo ikiwa ni sehemu ya mkakati wake wa kuwawezesha wadau wa sekta ya kilimo kuwa tayari kukopesheka ili kukuza shughuli zao za uzalishaji.