Joy FM
Joy FM
19 August 2026, 17:14

Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imeendelea kutoa elimu kwa wananchi ili waweze kujikinga na magonjwa ya mlipuko ikiwemo Ebola
Na Mwandishi wetu
Ukiwa ni mikakati wa Serikali kuimarisha utayari katika kudhibiti uwezekano wa magonjwa ya mlipuko kuingia nchini, Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwa kushirikiana na Wizara ya Afya wameongoza zoezi la ukaguzi wa maeneo tengefu kwa lengo la kutathmini utayari wa kukabiliana na ugonjwa wa Ebola.
Vituo hivyo ambavyo vimeandaliwa rasmi na Serikali, vimelenga kuimarisha nyanja za utoaji huduma za dharura kwa wagonjwa na wadhaniwa wa magonjwa ya milipuko ikiwemo Ebola.
Akizungumza baada ya ukaguzi wa kituo kimojawapo katika Hospitali ya Manispaa ya Kigoma/Ujiji ambayo ni miongoni mwa vituo tengefu kwa ajili ya kutoa huduma za dharura kwa magonjwa ya mlipuko, Mwakilishi kutoka Wizara ya Afya Dkt. Erick Richard amesema lengo la serikali ni kukagua, kutathmini na kubaini mapungufu katika vituo hivyo.

Amesema mapungufu yanayobainika yanafanyiwa kazi mara moja ili kuhakikisha ugonjwa huo hauingii nchini na iwapo utaingia udhibitiwe katika hatua za awali.
Ameongeza kuwa, tathmini na uboreshaji huo unafanyika katika mikoa yote nchi ambapo kwa sasa mikoa ya Kigoma na Kagera inaangaliwa kwa ukaribu kutokana na kuwepo katika mipaka ya nchi zinazotajwa kuathiriwa na magonjwa wa Ebola.
“pamoja na kuwajengea uwezo wataalam wetu, Wizara inasisitiza utayari katika kutekeleza afua mbalimbali za kudhibiti magonjwa ya milipuko ikiwemo Ebola” amesisitiza Dkt. Richard.
Dkt. Umoja Erasto Chona, ambaye ni Mratibu wa Matibabu Magonjwa ya mlipuko Mkoa wa Kigoma, amesema elimu imeendelea kutolewa kwa jamii kupitia makundi mbalimbali ikiwemo wazee maarufu, viongozi wa dini na wanahabari ili kuhakikisha jamii inajengewa uelewa na utayari ili kuchukua hatua dhigi ya ugonjwa wa Ebola iwapo utaingia nchini.