Joy FM
Joy FM
9 September 2024, 13:30

Mkuu wa wilaya Kasulu Kanali Isack Mwakisu amewataka vijana waliohitimu mafunzo ya awali ya kijeshi katika kambi ya 821 KJ Bulombora kujiepusha na matumizi ya madawa za kulevya kwani wanategemewa katika ujenzi wa taifa.
Na Josephine Kiravu – Kigoma
Vijana waliohitimu mafunzo ya awali ya kijeshi kwa mujibu wa Sheria operasheni miaka 60 ya Muungano kambi ya 821 Kj Bulombora wamehimizwa kutumia vyema ukuaji wa teknolojia pamoja na kuishi kiapo walichoapa wakati wa kuhitimu mafunzo hayo.
Hayo yameelezwa na Mkuu wa wilaya ya Kasulu Kanal Isaac Mwakisu kwa niaba ya mkuu wa Mkoa wa Kigoma Kamishna jenerali mstaafu wa jeshi la zimamoto na uokoaji Thobias Andengenye wakati wa kufunga mafunzo hayo ya awali ya kijeshi ambapo amesisitiza pia nidhamu na uadilifu kwa vijana hao.
Kwa upande wake mwakilishi wa Mkuu wa jeshi la kujenga Taifa nchini Kanal Ernest Sikaponda amewataka vijana hao waliohitimu kutumia vyema ujuzi walioupata huku akiwasihi kutojiingiza kwenye vikundi vya kihalifu.
Akisoma risala kwa mgeni rasmi mhitimu wa mafunzo ya kijeshi ya awali Veronica David wameshukuru kwa mafunzo waliyopata huku wakiiomba Serikali kuboresha upatikanaji wa huduma ya umeme kambini hapo.
Mafunzo ya awali ya kijeshi 821 KJ Bulombora yalianza kutolewa Juni 19 mwaka huu na kuhitimishwa hii leo.ambapo kwa mujibu wa Mkuu wa kikosi 821 KJ Bulombora Luteni Kanali Juma Hongo amesema baadhi ya vijana wameshindwa kuendelea na mafunzo kutokana na sababu mbalimbali.