Joy FM
Joy FM
6 July 2026, 11:56

Bei ya mazao ya kilimo ina mchango mkubwa katika maisha ya mkulima na maendeleo ya taifa kwa ujumla na miongoni mwa mazao hayo ni tumbaku, ambayo hulimwa katika baadhi ya maeneo nchini Tanzania na kuwa chanzo muhimu cha kipato kwa wakulima na mapato ya serikali.
Na Hagai Ruyagila
Wakulima wa zao la Tumbaku wilayani Kasulu mkoani Kigoma wameiomba Serikali kuangalia upya bei ya zao hilo ili iendane na gharama za uzalishaji na kuwawezesha kupata faida stahiki.
Wakizungumza na vyombo vya habari mji Kasulu, wakulima hao wamesema bei ya tumbaku imekuwa ikishuka katika misimu ya hivi karibuni, hali inayowaathiri kiuchumi na kupunguza motisha ya kuendelea kulima zao hilo.
Aidha, wameiomba serikali kushirikiana na wadau wa sekta ya tumbaku kutafuta suluhisho la kudumuu litakaloboresha mfumo wa bei na masoko ya zao hilo kwa manufaa ya wakulima.
Akizungumzia suala hilo, Katibu Tawala msaidizi uchumi uzalishaji mkoa wa Kigoma, James Peter amewasisitiza wakulima kuzalisha mazao hayo kulingana na mahitaji ya soko, huku akiwataka kuzingatia ubora wa mazao yao ili waweze kupata masoko maana serikali inadhamira ya kuhakikisha changamoto zinazowakabili wakulima zinatatuliwa na mazingira ya kilimo yanaendelea kuboreshwa kwa lengo la kuongeza tija na kuinua kipato chao.

Pia Peter amezungumzia namna ya kuimarisha uthibiti wa masoko ya mazao ya wakulima kwa kutenga maeneo maalum ya kuuzia mazao yao ili wakulima waweze kunufaika.