Joy FM
Joy FM
14 May 2026, 13:11

Serikali pamoja na wadau wa elimu wameendelea kuchukua juhudi mbalimbali za kuboresha sekta ya elimu nchini Tanzania na miongoni mwa juhudi hizo ni utoaji wa zana za ufundishaji na ujifunzaji
Na Tresipholi Odace
Walimu wakuu katika Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu wamepatiwa zana za ufundishaji na ujifunzaji pamoja na mafunzo maalumu kupitia program ya Memkwa iliyoko chini ya mradi wa elimisha mtoto ili kuhakikisha wanaongeza ufaulu mashuleni.
Akizungumza Afisa elimu Taaluma msingi Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu Bw. Michael Ngobe wakati wa mafunzo hayo ambayo yamelenga kuwajengea uwezo walimu juu ya namna ya kutengeneza zana za ufundishaji amesema kunakila sababu za kuhakikisha walimu wote katika halmashauri hiyo wanapatiwa mbinu bora za ufundishaji lengo ikiwa ni kuwajengea uwezo walimu wa Mpango wa Elimu Kwa Waliokosa yaani MEMKWA .
Aidha Bw Ngobe amehimiza walimu kutambua umuhimu wa kutunza takwimu ili kusaidia kupima matokeo ya matumizi ya zana za ufundishaji kwa watoto mashuleni.

Kwa upande wao washiriki wa mafunzo mmoja wao akiwa Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mvugwe Bi Marystella Ndigeza wamesema mafunzo hayo yatawasaidia kuongeza maarifa ya ufundishaji jambo litakalosaidia kuongeza ufaulu kwa wanafunzi.
Mafunzo haya yanayoendeshwa na Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu kwa kushirikiana na Shirika la Kimataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) yanalenga kuhakikisha walimu wanatambua umuhimu wa kufundisha kwa vitendo na kutumia mbinu za kisasa kufundishia ili kuongeza ufaulu mashuleni.