Joy FM
Joy FM
8 August 2026, 17:51

Maonesho ya wakulima maarufu nane nane yamefungwa rasmi leo ambapo wananchi wamepata nafasi ya kujifunza mambo mbalimbali ikiwemo teknolojia za kilimo huku Wilaya ya Uvinza ikiibuka kinara wa maonesho hayo kwa kundi la mamlaka ya serikali za mitaa
Na Mwandishi wetu
Mkoa wa Kigoma umeibuka mshindi katika maonesho ya wakulima 88 kanda ya magharibi kwa mwaka 2026 kwa kushika nafasi ya kwanza na ya pili leo Jumamosi Agosti 8, 2026 katika Viwanja vya Ipuli mkoani Tabora.

Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza imetangazwa kuwa mshindi wa 1 kwa kundi la mamlaka za Serikali za mitaa na Halmashauri ya Wilaya ya Buhigwe imeshika nafasi ya pili wakati Halmashauri ya Wilaya ya Igunga iliyopo Mkoa wa Tabora imeshika nafasi ya 3.
Mgeni rasmi, Mhe.Dr Jafar Rajab Seif, Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Afya) amekabidhi cheti cha ushindi, zawadi na Kikombe cha ushindi kwa mshindi wa kwanza na mshindi wa pili na kusisitiza kuwa maonesho ya wakulima ni darasa muhimu linalowapa fursa wakulima, wafugaji na wajasiriamali kutumia teknolojia hivyo waendelee kuzalisha bidhaa zenye ubora na viwango ili kukidhi soko la ndani na nje ya nchi.

“Yatumieni maonesho haya kuchota maarifa ya ufugaji bora na maabara za kilimo kwa kufuga kisasa, kutumia mbegu bora za mazao kwa manufaa yenu”, amesema Dr.Seif.

Aidha mgeni rasmi amesisitiza eneo la maonesho ya 88 kanda ya magharibi kuwa kituo cha ubora (center of excellence) na kuwaagiza Tanroads na Tarura kuweka miundombinu imara katika eneo hilo la maonesho Ipuli ili litumike mwaka mzima siyo wakati wa maonesho tu.
Aidha maonesho hayo yamehudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiongozwa na Kaimu mkuu wa Mkoa wa Tabora na Mkuu wa mkoa wa Kigoma, Balozi Simon Sirro, Viongozi wa Chama cha Mapinduzi, Wakuu wa Wilaya, makatibu Tawala na Wakurugenzi watendaji wa Kigoma na Tabora pamoja na wakuu wa Idara na Taasisi za Serikali.

Maonesho hayo yamefungwa rasmi leo Jumamosi Agosti 8, 2026 na Mhe.Dr Jafar Rajab Seif, Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Afya) ambaye alikuwa mgeni rasmi katika maonesho hayo ya wakulima kanda ya magharibi kwa mwaka 2026.