Joy FM

Vijana watakiwa kujikita katika kufaanya kazi Buhigwe

18 August 2026, 13:22

Afisa Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri ya Wilaya ya Buhigwe, Bi. Getruda Kibodi, Picha na Emman Kamangu

Vijana wameeleza kuwa baadhi yao wamekuwa wakikwepa kazi zinazohitaji juhudi kubwa na badala yake kutafuta kazi rahisi

Na Emmanuel Kamangu

Vijana katika Halmashauri ya Wilaya ya Buhigwe Mkoani Kigoma wametakiwa kuachana na tabia ya utegemezi na kujikita katika kufanya kazi ili kujikwamua kiuchumi na kujenga maisha yao ya baadaye.

Wito huo umetolewa na Afisa Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri ya Wilaya ya Buhigwe, Bi. Getruda Kibodi, ambapo amesema malezi kwa kiasi kikubwa yamechangia baadhi ya vijana kukua wakiwa na mtazamo wa kutegemea wengine badala ya kujituma na kutafuta fursa za kujiajiri.

“kiukwel hali hiyo inaweza kupunguza nguvu kazi katika jamii na kuongeza utegemezi miongoni mwa vijana wetu” amesema Kibodi.

Aidha, amewataka vijana kutumia vizuri fursa za mikopo inayotolewa na halmashauri, ikiwemo mikopo yenye riba ya asilimia nne, inayotokana na sehemu ya asilimia 10 ya mapato ya halmashauri inayotengwa kwa ajili ya kuwawezesha makundi mbalimbali.

Amesema mikopo hiyo inalenga kuwasaidia vijana kuanzisha na kuendeleza shughuli za uzalishaji, hivyo ni muhimu kuitumia kwa malengo yaliyokusudiwa ili iwe chanzo cha kipato na maendeleo.

Kwa upande wao, baadhi ya vijana wamesema kuna umuhimu wa kuchukuliwa hatua za haraka za kutoa elimu na kuwajengea vijana utamaduni wa kujitegemea. Wamesema kufanya hivyo kutawasaidia vijana wengi kujikita katika shughuli za uzalishaji na kuepuka kukaa vijiweni bila shughuli za kuwaingizia kipato.

Hata hivyo, vijana hao wameeleza kuwa baadhi ya wenzao wamekuwa wakikwepa kazi zinazohitaji juhudi kubwa na badala yake kutafuta kazi rahisi, jambo ambalo, kwa maoni yao, linaweza kuwanyima fursa ya kujenga uwajibikaji na msingi imara wa maisha yao ya baadaye.