Joy FM
Joy FM
19 September 2026, 10:27

Afya ni jambo muhimu katika maisha ya kila mwanadamu na ili jamii iwe na maendeleo, ni lazima watu wawe na afya njema na waweze kupata huduma za afya kwa urahisi
Na Mwandishi wetu
Timu ya Usimamizi na Uendeshaji wa Huduma za Afya (RHMT) Mkoa wa Kigoma imefanikiwa kutwaa tuzo katika kipengele cha Usimamizi Bora wa Huduma za Afya ya Msingi ngazi ya mikoa.

Tuzo hiyo imetolewa katika Mkutano wa Kimataifa wa Huduma za Afya ya Msingi, uliofanyika katika Kituo cha kimataifa cha mikutano jijini Arusha (AICC), Septemba 9 hadi 11,2026, ukiwa na lengo la kutathmini Maendeleo yaliyopatikana katika eneo la Afya ya Msingi, changamoto za upatikanaji wa rasilimali, kubadilishana uzoefu, ubunifu na kuboresha diplomasia ya Afya.
Akizungumza mara baada ya kukabidhiwa tuzo hiyo na Mwakilishi wa Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Katibu Tawala Mkoa wa Kigoma CPSP. Hassan Rugwa ameipongeza RHMT-Kigoma kwa utendaji kazi mzuri huku akisisitiza kuendelea kubaini changamoto za utoaji huduma katika Sekta hiyo na kuzitatua kwa wakati.

Upande wake Mwakilishi wa Mganga Mkuu Mkoa wa Kigoma Dkt. Albert Paschal, amesema kupitia Mkutano huo, yamefanyika makubaliano ya kuhakikisha huduma za Afya ya Msingi zinapaswa kuwa zenye usawa, gharama nafuu, zinazofikika, zenye ubora na zinazomweka mwanachi katikati ya huduma za Afya.
Mkutano huo ulifunguliwa na Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambapo katika tuzo hizo, mkoa umeshika nafasi ya tatu kimikoa kwa kigezo cha Usimamizi Bora wa Huduma za Afya ya Msingi.
