Joy FM

Viongozi wa kamati za mikopo ya 10% wafanya tathmini Uvinza

20 May 2026, 15:00

Viongozi wa kamati za mikopo ya asilimia 10 wakiwa katika kikao cha tathimini, Picha na Ofisi ya mawasiliano Uvinza

Kikao cha kamati za mikopo ya asilimia 10 husaidia kuhakikisha uwazi na usahihi katika utoaji wa mikopo kwani viongozi hupitia taarifa mbalimbali za vikundi na waombaji wa mikopo ili kuhakikisha fedha zinawafikia walengwa sahihi wenye sifa zinazotakiwa

Na Mwandishi wetu

Viongozi wa kamati ya mikopo ngazi ya Kata kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza Mkoani Kigoma wameshiriki katika Kikao cha tathmini ya mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na serikali kupitia Halmashauri.

Akifungua kikao hicho kilichofanyika katika ukumbi wa Halmashauri, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza Acland Kambili ameagiza ifikapo Julai Mosi Kila kata kutoa taarifa kamili juu ya ufuatiliaji wa mikopo hiyo marejesho ya vikundi nufaika.

Amesema kuwepo kwa taarifa sahihi kutasaidia kubaini Watendaji wanaofanya vizuri na kuwa mfano wa kuigwa kwa wengine.

Viongozi wa kamati za mikopo ya asilimia 10 wakiwa katika kikao cha tathimini, Picha na Ofisi ya mawasiliano Uvinza

Aidha, amewahimiza Watendaji Kata kufanya tafiti kwa kina zitakazowezesha kuibua vikundi vingi zaidi vitakavyonufaika hatua itakayochangia kupandisha idadi ya wanufaika katika makundi ya Vijana na wenye Ulemavu.

Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii Godfred Nkuba, amesisitiza kutokufanya kazi kwa mazoea akihimiza ushirikiano baina ya Watendaji na Vikundi husika ili kupata taarifa halisi za hali za vikundi na urejeshaji wa mikopo hiyo.

Akisoma miongozo mbalimbali ya utoaji wa mikopo ya Asilimia 10 mbele ya Watendaji hao, Afisa Maendeleo Ndg.Boniface Matete, amewakumbusha juu ya jukumu walilonalo katika kudhibiti mianya ya udanganyifu inayoweza kutumiwa na Wanavijundi wasiowaaminifu ili kuepuka usajili wa vikundi ghushi na vile vinavyokiuka taratibu za kiuendashaji kinyume na mradi ulioidhinishwa.

Viongozi wa kamati za mikopo ya asilimia 10 wakiwa katika kikao cha tathimini, Picha na Ofisi ya mawasiliano Uvinza

Zaidi ya shilingi milioni mia tatu arobaini 340,000,000/ zimetengwa katika robo ya nne ya mwaka ya mwaka wa fedha 2025/26 na tayari kwa vikundi kuwasilisha maombi katika Ofisi za serikali za mitaa zilizopo katika maeneo yao.