Joy FM
Joy FM
3 March 2026, 17:24

Kilimo cha tangawizi ni fursa nzuri kwa wakulima kutokana na soko lake kubwa na faida zake kiafya kwa kufuata kanuni bora za kilimo, mkulima anaweza kupata mavuno mengi na kuongeza kipato chake.
Na Michael Mpunije
Wakulima Wilayani Buhigwe Mkoani Kigoma wametakiwa kuongeza uwekezaji katika kilimo cha Tangawizi ili kunufaika na mpango wa Serikali wa kujenga kiwanda cha kuchakata zao hilo kinachotarajiwa kujengwa katika kata ya Munzeze wilayani humo.
Kilimo cha tangawizi ni miongoni mwa kilimo cha mazao ya biashara ambayo kwa wilaya ya Buhigwe kitovu cha zao hilo ni katika kata ya Munzeze na kwa kiasi kikubwa wakazi wa eneo hilo hutegemea sana kilimo hicho ukilinganisha na mazao mengine.

Akizungumza katika mkutano wa hadhara na wananchi wa kata ya Munzeze, Mbunge wa Jimbo la Buhigwe Prof. Pius Yanda amesema serikali imeweka mpango wa kujenga kiwanda cha kuchakata tangawizi ili kuwawezesha wananchi kuzalisha kwa tija.
Vijiji vya Kigogwe, Janda, Kirungu, Kinazi na Nyamihanga ni miongoni na maeneo yanayohimizwa kulima zao la tangawizi kutokana na mwitikio mdogo wa wananchi kulima zao hilo huku malengo makubwa ikiwa ni kuhakikisha kata zote za wilaya ya Buhigwe zinaanzisha kilimo hicho.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Kigogwe kata ya Munzeze Enock Ntahonsigaye amesema kilimo cha tangawizi kimekuwa na manufaa makubwa kwa wakazi wa kata hiyo licha ya uwepo wa changamoto mbalimbali huku wakiwa na matarajio makubwa baada ya ujenzi wa kiwanda hicho.
