Joy FM

Ujenzi MUHAS Kigoma wafikia 78.9%

10 June 2026, 14:54

Muonekano wa majengo ya MUHAS Kigoma ambapo ujenzi ukiendelea, Picha na Mwandishi wetu

Katibu tawala Mkoa wa Kigoma Hassan Rugwa amewataka wananchi wa Mkoa wa Kigoma kutoa ushirikiano na kulinda miradi ya maendeleo ambao inaendelea kutekelezwa

Na Mwandishi wetu

Ujenzi wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) Kampasi ya Kigoma, umefikia  Asilimia 78.9 huku ukitarajiwa kukamilika ifikapo Agosti,2026.

Muonekano wa majengo ya chuo cha afya MUHAS Kigoma, Picha na Mwandishi wetu

Kukamilika kwa ujenzi wa taasisi hiyo kunatoa fursa ya udahili wa kwanza kwa wanachuo watakaohitaji kusoma katika kampasi hiyo mwaka wa masomo 2026, jambo litakaloongeza fursa za kitaaluma kwa kada ya Afya na kuimarisha Sekta ya matibabu mkoani Kigoma na maeneo jirani.

Akizungumza mara baada ya kukagua Maendeleo ya ujenzi wa mradi huo, Katibu Tawala Mkoa wa Kigoma CPSP. Hassan Rugwa amesema kwa sasa Serikali inaendelea kukamilisha miundombinu muhimu ikiwemo barabara ili kulifanya eneo hilo kufikika kwa urahisi.

Katibu tawala Mkoa wa Kigoma akipokea maelezo baada ya kutembelea ujenzi wa MUHAS Kigoma, Picha na Mwandishi wetu

Amesema Taasisi hiyo ni kiungo muhimu hivyo wakazi wanapaswa kuchangamkia fursa mbalimbali zitakazojitokeza kutokana na uwepo wa chuo hicho.

Naye Mhandisi Mkazi wa mradi huo Selemani Malambo, amesema kazi zote za msingi katika ujenzi huo zimekamilika huku zikibaki kazi chache za ukamilishaji wa miundombinu ya ndani sambamba na usawazishaji wa ardhi nje ya majengo hayo.

Muonekano wa majengo katika ujenzi wa chuo cha MUHAS Kigoma, Picha na Mwandishi wetu