Joy FM
Joy FM
5 August 2026, 14:01

Uhamiaji haramu ni kitendo cha mtu kuingia, kuishi au kufanya kazi katika nchi fulani bila kufuata taratibu na sheria zilizowekwa na nchi hiyo na tatizo hili limekuwa katika sehemu mbalimbali duniani kutokana na sababu kama vile ukosefu wa ajira, umaskini, migogoro ya kisiasa na kutafuta maisha bora
Na Hagai Ruyagila
Wananchi wa Kata ya Nyamnyusi, Halmashauri ya Wilayani Kasulu Mkoani Kigoma, hususan wakazi wa Kitongoji cha Muhanga, wametakiwa kuzingatia sheria, taratibu na kanuni za uhamiaji wanapowapokea wageni kutoka nchi jirani, ili kusaidia kudhibiti na kutokomeza tatizo la uhamiaji haramu.
Wito huo humetolewa na Polisi Kata wa Kata ya Nyamnyusi, Mkaguzi Msaidizi wa Polisi Willy Lupa, Wakati akizungumza na wananchi wa Kitongoji cha Muhanga, Kijiji cha Mkieta, katika Halmashauri ya wilaya ya Kasulu.
Amesema serikali itaendelea kushirikiana kwa karibu na wananchi katika mapambano dhidi ya uhamiaji haramu, akisisitiza kuwa kila mwananchi ana wajibu wa kutoa taarifa kwa mamlaka husika pale atakapobaini uwepo wa wahamiaji haramu, ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa kwa wakati.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Mkieta, Hassan Kisema, amewasisitiza wananchi kuzingatia maelekezo yaliyotolewa na Polisi Kata, akieleza kuwa unappomkaribisha muhamiaji haramu si jambo jema maana anaweza kusababisha changamoto hivyo ushirikiano kati ya wananchi na vyombo vya ulinzi na usalama utasaidia kuimarisha amani na usalama wa kijiji pamoja na kuzuia changamoto zinazoweza kusababishwa na uhamiaji haramu.

Baadhi ya wananchi wa Kitongoji cha Muhanga wameahidi kuendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa wanapobaini viashiria vya uhamiaji haramu, huku wakimpongeza Mkaguzi Msaidizi wa Polisi Willy Lupa kwa ushirikiano wake wa karibu na wananchi katika kuimarisha usalama wa raia na mali zao.