Joy FM

Mikopo ya 10% ilivyowainua wanawake Kigoma DC

30 September 2026, 15:53

Baadhi ya wanafaika wa mikop ya asilimia 10 katika Halmashauri ya Wilaya Kigoma, Picha na Lucas Hoha

Mkiopo ya asilimia kumi inayotolewa na halmasahauri kupitia mapato ya ndani imeendelea kuwasaidia wananchi hasa vikundo vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu

Na Lucas Hoha

Idara ya Maendeleo ya Jamii katika Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma imetembelea na kukagua maendeleo ya vikundi mbalimbali vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu vilivyonufaika na mikopo inayotokana na asilimia 10 ya mapato ya ndani ya Halmashauri.

Lengo la ziara hiyo ni kuhamasisha wanufaika kutumia mikopo hiyo kwa ufanisi, kufanya kazi kwa bidii na kutambua mchango wa Serikali katika juhudi za kuwawezesha wananchi kujikwamua kiuchumi.

Baadhi ya wanufaika wa mikopo kutoka katika vikundi mbalimbali vilivyotembelewa na idara ya Maendeleo ya Jamii katika Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma, wakieleza namna mikopo hiyo ilivyowawezesha kuanzisha na kuendeleza shughuli zao za kiuchumi.

Miongoni mwa vikundi vilivyotembelewa ni Kikundi cha Wanawake cha Ilakoze Nyamuhoza, ambacho kimepatiwa mkopo wa shilingi milioni 20 kwa ajili ya kuanzisha kiwanda cha kuchakata mafuta ya mawese.

Kikundi hicho sasa kinaendelea na shughuli za uzalishaji, kama anavyoeleza Mwenyekiti wa kikundi hicho, Ileni Dismas.

Aidha, Idara hiyo imetembelea Kikundi cha Vijana cha Youth Group Mjimwema, kilichopo Kata ya Mahembe, ambapo wanachama wake wameeleza kuwa mikopo hiyo imewapa fursa ya kujiajiri na kuendesha shughuli mbalimbali za kiuchumi.

Kwa upande mwingine, baadhi ya vikundi vya Watu wenye Ulemavu vilivyotembelewa vimeishukuru Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma kwa kuwaamini na kuwawezesha kupata mikopo, wakisema fursa hiyo imewasaidia kushiriki katika shughuli za kiuchumi na kujikwamua kiuchumi.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Afisa Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma, George Vangisaul, amesema Halmashauri imeendelea kutoa mikopo kwa makundi ya Wanawake, Vijana na Watu wenye Ulemavu bila ubaguzi.

Amesema Halmashauri itaendelea kuratibu na kutenga fedha kwa ajili ya kuwawezesha wananchi kupitia mikopo hiyo.

Ziara hiyo imefanyika katika maadhimisho ya Wiki ya Maendeleo ya Jamii nchini Tanzania, ambapo Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma imeadhimisha wiki hiyo kwa kutembelea na kukagua miradi mbalimbali inayotekelezwa na wanufaika wa mikopo inayotokana na mapato ya ndani ya Halmashauri.