Joy FM

Tamasha la BUHA 2026 kuwaunganisha wana Kigoma

6 October 2026, 13:48

Baadhi ya viongozi wakizungumza na wanahabari kuelekea uzinduzi wa tamasha la BUHA 2026, Picha na Orida Sayon

Tamasha la BUHA 2026 linatarajiwa kufanyika Disemba 2026 likiwa na lengo la kuenzi mila na desturi za watu wa Kigoma na elimu mbalimbali ya uraia

Na Orida Sayon

Wananchi Mkoani Kigoma wametakiwa kushiriki tamasha la Buha 2026 jukwaa linalolenga kujenga mahusiano, ushirikiano na maendeleo ya jamii na kuenzi urithi wa Buha.

Tamasha hili limeandaliwa na umoja wa Ibhuha Yachu likiwa na lengo la kuwakutanuisha waha wanaoishi katika maeneo mbalimbali ya Tanzania na nje ya nchi ili kuenzi urithi wa buha na  kujadili mshikamano katika kuchangia maendeleo ya mkoa wa kigoma.

Akizungumza na wandishi wa habari Mkoani kigoma Mwenyekiti wa kamati ya maandalizi ya tamasha la Buha 2026 Stewart  Ernest  Zindutse  amesema urithi wa buha ni sehemu ya utajiri katika utamaduni wa Tanzania hivyo tamashaa hilo linakusudiwa  kuwa jukwaa la kutangaza  lugha, historia, mila na desturi kuendelea kurithishwa kizazi hadi kizazi.

Zindutse amesema tamasha  hilo linatoa fursa kwa wajasiriamali, vikundi vya wanawake na vijana, wasanii na wafanyabiashara kuonyesha bidhaa na kazi zao.

Naye  Dr. Peter Mayengo ambaye pia ni mjumbe wa kamati ya maandalizi ya tamasha hilo amesema licha ya kutangaza na kuenzi urithi wa tamaduni za buha vijana watakuwa na nafasi ya kujifunza fursa zinazopatikana katika matumizi ya teknolojia kujiongezea kipato

Aidha Mwenyekiti kamati ya habari na mawasiliano wa umoja wa Buha Yetu Prosper Kwigize amesema pia wanakigoma watapata fursa ya elimu ya uraia na uzalendo katika tamasha hilo.

Tamasha la Buha 2026 linatarajiwa kufanyika kuanzia Desemba 17-19 2026 likiwa na kaulimbiu ya “Tukumbuke asili, Tujenge Umoja na Maendeleo” hivyo waha wanaoiishi Tanzania na nje ya Tanzania, wasanii, wanazuoni, taasisi binafsi na za umma hawana budi kushiriki.