Joy FM
Joy FM
21 August 2026, 10:56

Ulinzi shirikishi ni jukumu la mwananchi katika kuhakikisha vitendo vya wizi, udokozi na uporaji vinakomeshwa kwenye jamii na kuchochea maendeleo
Na Hagai Ruyagila
Uwepo wa kikundi cha ulinzi shirikishi katika Kata ya Murusi, Halmashauri ya Mji Kasulu mkoani Kigoma, umeendelea kusaidia kuimarisha hali ya ulinzi na usalama pamoja na kurejesha utulivu kwa wananchi wa kata hiyo.
Hayo yamebainishwa na Diwani wa Kata ya Murusi, Mheshimiwa Elisha Bakena, wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake.

Mhe. Bakena amesema vitendo vya uhalifu na uvunjifu wa amani vilikuwa miongoni mwa changamoto zilizokuwa zikikabili kata hiyo, hali iliyosababisha baadhi ya wananchi kuishi kwa hofu na kukosa amani.

Amesema kupitia ushirikiano baina ya viongozi wa kata, Jeshi la Polisi, wananchi pamoja na vijana wa ulinzi shirikishi, wamefanikiwa kukabiliana na changamoto hizo, na kwa sasa hali ya usalama imeimarika na amani imerejea katika mitaa yote ya Kata ya Murusi.
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Kikoba, Robert Petro, amesema kuanzishwa kwa kikundi cha ulinzi shirikishi katika mtaa huo kulitokana na kuwepo kwa changamoto ya vitendo vya uhalifu, hali iliyohitaji ushirikiano wa wananchi katika kulinda usalama wa eneo lao.

Mwenyekiti wa serikali ya mtaa wa Kikoba Robert Petro, Pucha na Hagai Ruyagila
Naye Kiongozi Msaidizi wa Ulinzi Shirikishi katika Mtaa wa Kikoba, Sabiti Paulo, amesema wanaendelea kushirikiana na vijana, wananchi pamoja na viongozi wa maeneo yao kuhakikisha vitendo vya uhalifu vinadhibitiwa na amani inaendelea kutawala.
Ameongeza kwa kuushukuru uongozi wa Kata ya Murusi kwa kuanzisha kikundi hicho, akisema hatua hiyo imekuwa na mchango mkubwa katika kuwawezesha wananchi kuendelea kudumisha amani na usalama katika maeneo yao.