Joy FM
Joy FM
16 September 2026, 14:43

Asilimia 30 inalenga kuhakikisha makundi hayo hayabaki watazamaji katika matumizi ya fedha za Serikali, bali yanashiriki moja kwa moja kama wazabuni na watoa huduma
Na Emmanuel Kamangu
Taasisi za ununuzi za Serikali katika Kanda ya Magharibi zimetakiwa kuhakikisha zinazingatia matakwa ya kisheria kwa kutoa fursa kwa makundi maalumu kunufaika na zabuni zinazotekelezwa katika maeneo mbalimbali.
Akizungumza na Radio Joy, Meneja wa Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) Kanda ya Magharibi, Mhandisi Suma Mwanjwango, amesema baadhi ya taasisi za Serikali, ikiwemo halmashauri, zimekuwa zikikiuka matakwa ya kisheria yanayozitaka kutenga asilimia 30 ya zabuni kwa ajili ya makundi maalumu.
Amesema makundi hayo ni wanawake, vijana, wazee na watu wenye ulemavu, huku akieleza kuwa utaratibu huo ni sehemu ya mpango wa Serikali wa kuwawezesha makundi hayo kujikwamua kiuchumi.

Mhandisi Mwanjwango amezitaka halmashauri kutambua na kuainisha kazi zinazoweza kutekelezwa na makundi maalumu ili kuhakikisha yanapata fursa ya kushiriki katika zabuni mbalimbali zinazotolewa na taasisi za umma.
Aidha, amesema PPRA inaendelea kufanya mazungumzo na taasisi za kifedha kwa lengo la kushirikiana katika kuwawezesha wanufaika wa mpango huo kupata mitaji mikubwa itakayowawezesha kushiriki na kutekeleza zabuni kwa ufanisi.
Amesema mamlaka ya udhibiti wa ununuzi wa umma (PPRA) imekuwa ikiendelea kutoa elimu kwa taasisi za umma kuhusu umuhimu wa kuzingatia utaratibu wa kutenga asilimia 30 ya bajeti ya manunuzi kwa ajili ya wanawake, vijana, wazee na watu wenye ulemavu, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuwawezesha kiuchumi.