Joy FM

Madereva, wafanyabiashara wakosa huduma ya choo Kigoma

7 October 2026, 15:13

Muonekano wa makopo ya mikojo ya madereva na wafanyabiashara mjini Kigoma baada ya kukosa choo, Picha na Mwandishi wetu

Wamesema ukosefu wa choo unaweza kusababisha magonjwa ya mlipuko kutokana na qengi wao kujisaidia haja ndogo kwenye makopo ya maji

Na Mwandishi wetu

Baadhi ya Madereva wa vyombo vya moto katika Standi ya magari ya Stesheni Manispaa ya Kigoma Ujiji wameilalamikia serikali kushindwa kurejesha huduma ya Choo katika eneo hilo baada ya choo kilichokuwa kinatumika kufungwa kwa zaidi ya miezi Miwili kutokana na kukosekana kwa huduma ya Maji.

Muonekano wa choo kilchokuwa kinatumika awali kabla ya kufungwa na kusababisha huduma kukosa, Picha na Mwandishi wetu

Wakizungumza na Radio Joy Fm baadhi ya Madereva hao wametaja adha wanayopitia wakati wanapohitaji huduma ya Choo ambapo baadhi yao wanalazimika kusafiri kwenda Mwanga Sokoni kufuata huduma ya choo, huku wakiomba Uongozi wa Manispaa ya Kigoma Ujiji kuwasaidia kutatua kero hiyo.

Baadhi wa madereva na wafanyabiashara, Picha na mwandishi wetu

Kwa Upande wao baadhi ya Wafanyabiashara wa maeneo hayo wamesema changamoto hiyo ni ya muda sasa na inawaathiri Wafanyabiashara hao kwani wanapofuata huduma ya Choo umbali mrefu wanalazimika kufunga biashara, nakuwa wamekuwa wakishuhudia baadhi ya watu wasiowaaminifu wakijisaidia kwenye mitaro iliyopo Maeneo hayo.

Akijibu malalamiko hayo, Afisa usafi wa mazingira Manispaa ya Kigoma Ujiji Bi. Petronila Gwakila amesema Choo hicho kilifungwa kwa sababu kilikuwa kibovu na kuwa tayari kuna mdau wamempata ili abomoe Choo hicho na kukijenga upya