Joy FM

Mradi wa Ebola preparedness & protection watambulishwa Uvinza

1 October 2026, 07:34

Baadhi ya viongozi wakiwa katika uzinduzi wa mradi wa kukabiliana na ebola, Picha na Mwandishi wetu

Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo wameendelea kuweka mikakati na elimu kwa wananchi juu ya namna ya kujikinga na ebola

Na Mwandishi wetu

Mradi wa Ebola Preparedness & Protection Project umetambulishwa rasmi katika Wilaya ya Uvinza, Mkoa wa Kigoma, ukiwa na lengo la kuimarisha utayari na hatua za kinga dhidi ya ugonjwa wa Ebola.

Mradi huo ulitambulishwa rasmi mkoani Kigoma tarehe 16 Septemba 2026, na sasa umeanza kutambulishwa katika Wilaya ya Uvinza katika kata za Herembe, Igalula na Buhingu ili kuwafikia wadau na jamii katika maeneo yenye uhitaji wa kuongeza uelewa na maandalizi dhidi ya Ebola.

Mradi unatekelezwa na ActionAid Tanzania kwa kushirikiana na Disability Relief Services Tanzania (DRST), chini ya ufadhili wa wadau wa maendeleo.

Mradi huo umeanzishwa kutokana na wasiwasi wa uwezekano wa kuenea kwa ugonjwa wa Ebola kutoka nchi jirani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

Mkoa wa Kigoma unatambuliwa kuwa eneo lenye hatari kubwa kutokana na mwingiliano mkubwa wa kijamii na kibiashara pamoja na uwepo wa harakati za watu, ikiwemo wakimbizi, hali inayohitaji kuimarishwa kwa uelewa, tahadhari na maandalizi ya kukabiliana na Ebola.