Joy FM
Joy FM
16 July 2026, 16:22

Malaria ni miongoni mwa magonjwa yanayoendelea kuwa tishio kubwa kwa afya ya jamii, hususan katika nchi za Afrika zikiwemo Tanzania na ugonjwa huu husababishwa na vimelea vinavyosambazwa kupitia mbu aina ya Anopheles
Na Emmanuel Kamangu
Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma imepokea lita 2,610 za viuadudu vya kudhibiti mazalia ya mbu kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, zenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 31. Hatua hiyo ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuhakikisha ugonjwa wa malaria unatokomezwa ifikapo mwaka 2030.
Akizungumza wakati wa kupokea viuadudu hivyo pamoja na ufunguzi wa mafunzo maalumu kwa wataalamu wa afya na wahudumu wa afya ngazi ya jamii kuhusu namna ya kudhibiti mazalia ya mbu, Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu, Dkt. Chacha Turubeti, amewataka washiriki kutumia elimu na vifaa walivyopatiwa kwa ufanisi ili kufanikisha mapambano dhidi ya malaria na kuleta matokeo chanya kwa jamii.

Kwa upande wake, Mratibu wa Kudhibiti Ugonjwa wa Malaria katika Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu, Dkt. Berlino Mlange, amesema lengo la utekelezaji wa zoezi la unyunyiziaji wa viuadudu katika mazalia ya mbu ni kupunguza kwa kiwango kikubwa maambukizi ya malaria na kuhakikisha wananchi wanakuwa salama dhidi ya ugonjwa huo. Ameongeza kuwa zoezi hilo litatekelezwa kwa kuendelea katika maeneo mbalimbali ya halmashauri.
Naye mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo na Mhudumu wa Afya Ngazi ya Jamii, Bi. Belenadeta Asheri, amesema mafunzo hayo yamewaongezea uelewa na uwezo wa kitaalamu katika kutambua na kudhibiti mazalia ya mbu, jambo litakalosaidia kuboresha huduma za kinga dhidi ya malaria kwa wananchi.
Wakati huohuo, wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu wametakiwa kutoa ushirikiano kwa wataalamu wa afya watakapofika katika maeneo yao kutekeleza zoezi la unyunyiziaji wa viuadudu kwenye mazalia ya mbu, ili kuimarisha juhudi za Serikali za kutokomeza malaria na kufanya ugonjwa huo kuwa historia nchini.