Joy FM
Joy FM
24 July 2026, 14:06

Mpango wa mikopo ya asilimia 10 umeendelea kuwa chachu ya maendeleo ya vikundi kwa kuongeza mtaji, kuimarisha shughuli za kiuchumi, kuongeza ajira na kipato cha wanachama, pamoja na kuboresha ustawi wa familia na jamii kwa ujumla.
Na Hagai Ruyagila
Halmashauri ya Mji Kasulu mkoani Kigoma imetenga zaidi ya shilingi milioni 200 kwa robo ya kwanza ya Mwaka wa fedha 2026/2027 kwa ajili ya mikopo ya asilimia 10 kwa vikundi vya wanawake, Vijana na Watu wenye ulemavu ili kuwawezesha kujikwamua kiuchumi kupitia shughuli mbalimbali za uzalishaji.
Akizungumza na vyombo vya habari, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mji Kasulu, Mwl. Vumilia Simbeye, amesema halmashauri hiyo tayari imefungua dirisha la mikopo hiyo kwa mwaka wa fedha 2026/2027 ikiwa ni utekelezaji wa maagizo ya Serikali kwa halmashauri kutenga asilimia 10 ya fedha zinazotokana na mapato ya ndani ya halmashauri kwa ajili ya vikundi mbalimbali.
Mwl. Simbeye amesema kutengwa kwa zaidi ya shilingi milioni 200 kwa Mwaka huu wa fedha kunatoa fursa kwa wananchi wengi zaidi kunufaika na mikopo hiyo. Akisisitiza wananchi kujiunga katika vikundi vinavyotambulika na kujitokeza kuomba mikopo hiyo.
Aidha Mwl Simbeye amesema kwa Mwaka wa fedha uliopita 2025/2026 Halmashauri hiyo imetoa mikopo ya zaidi ya shilingi milioni 600 kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.
Mratibu wa mikopo ya asilimia kumi inayotolewa na Vijana, Wanawake na Watu wenye ulemavu Halmashauri ya Mji Kasulu, Godfrey Jeremiah, amezungumzia sifa zinazotakiwa kwa waombaji wa mikopo hiyo ikiwemo kuwa na namba ya nida.

Baadhi ya wananchi wa Halmashauri ya Mji Kasulu wameipongeza Serikali kwa kuendelea kutenga fedha za mikopo ya asilimia 10, wakisema mpango huo umekuwa chachu ya kuanzisha na kupanua shughuli za kiuchumi, kuongeza kipato cha kaya na kuboresha ustawi wa familia zao.