Joy FM
Joy FM
1 June 2026, 14:35

Kambi ya madaktari ni mpango wa muda mfupi unaowaleta wataalamu wa afya katika jamii ili kutoa huduma za matibabu, uchunguzi na elimu ya afya na kambi hizi zina umuhimu mkubwa katika kuboresha afya ya wananchi, hasa katika maeneo ya vijijini ambako huduma za afya ni chache
Na Timotheo Leonard
Zaidi ya wananchi elfu mbili na mia tano Mkoani Kigoma, wanatarajia kunufaika na kambi ya siku tano ya madaktari bingwa na ubingwa bobezi inayolenga kusogeza huduma za kibingwa karibu na jamii.
Kambi hiyo imezinduliwa rasmi leo Juni Mosi, 2026 katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kigoma Maweni, na Katibu Tawala wa Mkoa Hassan Rugwa, ambapo itahitimishwa tarehe tano Juni 2026.

Rugwa amebainisha kuwa uwepo wa kambi hiyo utasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza usumbufu na gharama kwa wananchi, ambao walilazimika kusafiri umbali mrefu kufuata huduma hizo mikoa mingine ikiwemo Dodoma na Dar es Salaam.
Kwa upande wake, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Maweni, Daktari Joseph Nangawe, amewataka wananchi kuchamkia fursa hiyo adhimu, huku akifafanua kuwa kambi hizo zimekuwa zikiendeshwa kila robo mwaka na zimeleta matokeo chanya.
Nao baadhi ya wananchi waliojitokeza kupata matibabu hayo, wameishukuru serikali kwa kusogeza huduma hizo mlangoni mwao, wakisema hatua hiyo imewaokoa na safari ndefu za kutafuta matibabu.
Kambi ya madaktari ni mpango wa muda mfupi unaowaleta wataalamu wa afya katika jamii ili kutoa huduma za matibabu, uchunguzi na elimu ya afya na kambi hizi zina umuhimu mkubwa katika kuboresha afya ya wananchi, hasa katika maeneo ya vijijini ambako huduma za afya ni chache.