Joy FM
Joy FM
1 June 2026, 12:44

Hedhi ni mchakato wa kawaida wa kibaiolojia unaowapata wasichana wanapofikia umri wa balehe ingawa ni jambo la kawaida na muhimu kwa afya ya uzazi, hedhi inaweza kuwa changamoto kwa baadhi ya watoto wa kike kutokana na ukosefu wa elimu sahihi, vifaa vya usafi, na mazingira rafiki
Na Tryphone Odace
Wasichana waishio maeneo ya vijijini wilayani Uvinza mkoani Kigoma, wamesema upatikanaji wa taulo za kike pamoja na miradi mingine inayolenga kutoa huduma za afya ya uzazi kwa vijana ni hatua muhimu katika kuwawezesha kufikia ndoto zao sawa na wasichana wa maeneo ya mijini ambako huduma hizo hupatikana kwa urahisi.
Hayo yameelezwa na wasichana wa shule ya Sekondari Kalya iliyoko kijiji cha Tamusha Kata ya Kalya Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma, mara baada ya kupokea vifaa vya kujisitiri kipindi cha hedhi ikiwemo taulo za kike na nguo za ndani na sabuni, vilivyotolewa na Shirika la Maendeleo ya Vijana Tanzania Restless Development, chini ya ufadhili wa UNICEF na Global Affairs Canada.
Miongoni mwa wasichana hao ni Mlezi Selemani na Yusta Emmanuel, ambao wamesema suala la hedhi limesababisha baadhi ya wasichana kukosa vipindi darasani na wengine hata kukatisha kabisa masomo yao kutokana na ukosefu wa huduma za hedhi salama.
John Yohaness Maftah ni Mratibu wa Mradi wa Elimu kwa Watoto na Vijana Balehe waishio katika mazingira hatarishi, amesema kulingana na tafiti, ukosefu wa vifaa vya kujisitiri na ukosefu wa vyumba salama vya wasichana kujisitiri shuleni husuan maeneo ya vijijini, vinachangia pakubwa utoro kwa wanafunzi wa kike, huku Afisa Elimu, Elimu ya Watu Wazima mkoa wa Kigoma Bi. Fausta Wilbard, akisisitiza kuwa wadau wote wana nafasi muhimu kwenye suala la hedhi kwa wasichana.
Mratibu wa Mradi wa Elimu kwa Watoto na Vijana Balehe waishio katika mazingira hatarishi katika Kata ya Kalya wilayani Uvinza, Masaka Hussein, amesema takribani wanafunzi 200 hadi 300 wakiwemo wavulana na wasichana kwa vpindi tofauti kila mwezi hawahdhurii shule huku moja ya sababu ikiwa ni suala la hedhi.