Joy FM

Joy Fm yaadhimisha miaka 10 kwa kupanda miti Kigoma

30 April 2026, 13:05

Muonekano wa miche ya miti inayopandwa na Redio Joy Fm kama sehemu ya maadhimisho ya miaka 10 tangu kuanzishwa kwake, Picha na Esperencer Ramadhan

Tukio hilo limebeba ujumbe mzito wa utunzaji wa mazingira na uhamasishaji wa jamii kushiriki katika kupambana na mabadiliko ya tabianchi

Na Mwandishi wetu

Katika kuadhimisha miaka kumi tangu kuanzishwa kwa Redio Joy FM, uongozi wa redio hiyo umeungana na viongozi wa serikali na taasisi za mazingira katika zoezi la upandaji miti lililofanyika katika Shule ya Msingi Matyazo Kalinzi Halmashauri ya Wilaya Kigoma.

Muonekano wa bango la Redio Joy Fm, likionyesha ujumbe wa kuadhimisha miaka 10 ya kuanzishwa kwake, Picha na Esperancer Ramadhan

Akizungumza katika hafla hiyo, Meneja wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Kanda ya Magharibi Edgar Mgila amesisitiza umuhimu wa kupanda miti kama njia mojawapo ya kulinda mazingira na kuhakikisha uwepo wa hewa safi kwa vizazi vijavyo.

Aidha ameeleza kuwa ushiriki wa taasisi binafsi kama Joy FM ni mfano mzuri wa kuigwa katika juhudi za kuhifadhi mazingira.

Kwa upande wake, Katibu tawala Wilaya Kigoma Mganwa Nzota ameipongeza Redio Joy FM kwa hatua hiyo, akieleza kuwa maadhimisho hayo yamekuwa na tija kubwa kwa jamii badala ya kuwa ya sherehe pekee huku akihimiza wananchi, hasa wanafunzi, kuthamini miti inayopandwa kwa kuitunza ili iweze kukua na kutoa manufaa yaliyokusudiwa.

Katibu tawala Wilaya Kigoma akizungumza wakati wa hafla ya upandaji miti shule ya msingi Matyazo wakati Joy Fm ikiadhimisha miaka 10 kuanzishwa kwake, Picha na Esparencer Ramadhan

Naye Mkurugenzi wa Redio Joy FM, Mwenge Muyombi amesema kuwa katika kusherehekea miaka kumi ya mafanikio, redio Joy Fm imeona ni vyema kurejesha kwa jamii kwa vitendo ikiwemo kupanda miti pamoja matukio mbalimbali yatayoendelea baada ya uzinduzi wake.

Ameongeza kuwa Joy FM itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuendesha kampeni za mazingira na maendeleo ya kijamii.

Sauti ya lisala ya upandaji miti ikisoma na Sekretari wa Joy Fm Maria Buremo
Afisa Misitu TFS Pendo Macha akizungumza wakati ya maadhimisho ya miaka 10 tangu kuanzishwa kwake, Picha na Esperancer Ramadhan

Zoezi hilo limeehusisha upandaji wa miche ya miti ya zaidi ya mia mbili katika shule yamsingi Matyazo, huku wanafunzi, walimu, na wananchi wakishiriki kwa hamasa kubwa na maadhimisho hayo yameacha alama chanya katika shule hiyo, huku yakitoa somo muhimu juu ya wajibu wa kila mmoja katika kulinda mazingira.